Samatta aivaa Napoli akisaka rekodi ya kutisha Ligi ya Mabingwa

Monday December 9 2019

Mwanaspoti-Samatta-aivaa-Napoli-akisaka-Tanzania-rekodi-kuzifunga-timu-zote-Kundi E

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Mbwana Samatta anayeichezea klabu ya KRC Genk,  atakuwa na kibarua kizito usiku wa kesho nchini Italia  cha kufukuzia rekodi ya kuzifunga timu zote Kundi E  katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Samatta anatarajiwa kuiongoza KRC Genk nchini humo majira ya saa 2:55 usiku kwa saa za Afrika Mashariki  katika mchezo ambao kwao ni wa kukamilisha ratiba ya hatua ya makundi dhidi ya  Napoli kwenye uwanja wa San Paolo wenye uwezo wa kuingiza watazamaji, 55, 000.

Katika mchezo huo, Samatta anatarajiwa kukutana na upinzani mkali kutoka kwa mabeki wa Napoli, wakiongozwa na Msenegal, Kalidou Koulibaly kutokana na umuhimu wa mchezo huo kwao ambao utatoa picha ya nafasi ambayo wanaweza kumaliza katika kundi hilo.

Kwa mara ya kwanza Samatta kucheza dhidi ya Napoli, ilikuwa Oktoba 2 wakiwa nyumbabni kwao Ubelgiji, walitoka nao suluhu, mshambuliaji huyo wa Kitanzania, alionekana kudhibitiwa na Msenegal huyo ambaye alicheza beki wa kati sambamba na Mgiriki, Konstantinos  Manolas.

Kama Samatta atafunga mbele ya mabeki hao bora, atakuwa ameweka rekodi ya kuzifunga klabu zote ambazo walipangwa nazo katika kundi E.

Akiuzungumzia mchezo huo, Samatta mwenye mabao matatu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, alisema, "Mechi kiukweli itakuwa ngumu kwa sababu Napoli ni miongoni mwa klabu kubwa Ulaya, ambazo zimekuwa na Historia kubwa na mashindano haya.

Advertisement

"Kwa namna ambavyo tumejiandaa, tutajaribu kadri ambayo itawezekana kuona kama tunaweza kumaliza vizuri mashindano haya ambayo yametupa somo wengi wetu ambao hii ni mara yetu ya kwanza kucheza."

Samatta mwenye mabao saba katika michezo 17 ya Ligi Kuu Ubelgiji, alifungua akaunti yake ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Septemba 17 nchini Austria ambako licha ya kupoteza kwa mabao 6-2 mbele ya Salzburg, alifunga bao lake la kwanza dakika ya 52.

Kucheza tu mchezo huo kwa Samatta ilikuwa rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza michuano hiyo mikubwa Ulaya ngazi ya klabu na alipofunga akajiwekea rekodi nyingine ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kufunga katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baada ya mchezo huo, wakatoka suluhu na Napoli, uliofuata wakachapwa na Liverpool kwa mabao 4-1 na bao lake lilikataliwa katika mchezo huo na VAR, lakini katika mchezo wa marudiano nchini England, aliifunga Anfield pamoja na kuwa walipoteza kwa mabao 2-1.

Bao la tatu la Samatta katika mashindano hayo, alifunga tena dhidi ya Salzburg,Novemba 27 katika mchezo huo walipoteza kwa mabao 4-1 wakiwa nyumbani.

Wakati Napoli wenye pointi tisa wakicheza dhidi ya Genk yenye pointi moja, Liverpool wenye pointi 10 watakuwa Austria kucheza na Salzburg wenye pointi saba ambao kimahesabu nao  bado wananafasi  ya kutinga hatua ya mtoano.

Michezo mingine ambayo inatarajiwa kuchezwa kesho katika usiku wa Ulaya kutoka kundi F, Borussia Dortmund wenye pointi saba watacheza dhidi ya Slavia Prague wenye pointi mbili, Inter Milan yenye pointi saba pia watacheza dhidi ya FC Barcelona ambayo inatiketi ya kuingia mtoano. Katika kundi hilo kazi ipo kwa Dortmund na Inter.

Kund G, Benfica watacheza dhidi ya Zenit St. Petersburg huku Lyon dhidi ya Leipzig. Zenit au Lyon mmoja wapo anaweza kuungana na Leipzig wenye pointi 10 kutokana na wote wawili kila mmoja kuwa na pointi saba.

Kitendawili kingine katika Kundi H ambalo tayari Ajax wanatiketi ya kuingia mtoano, miamba hiyo ya soka la Uholanzi watacheza dhidi ya Valencia wenye pointi nane  sawa na Chelsea ambao watacheza dhidi ya Lille.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisement