SOYA Awards: Ouma Vs Bitok ni mambo mbaya!

Muktasari:

David Ouma na Paul Bitok, wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa Alex Alumirah (Vihiga Queens), Carey Odhiambo (Morans) na Curtis Olago (KCB RFC).

Nairobi. Kocha wa Harambee Starlets, David Ouma na mwenzake wa timu ya wanawake ya mchezo wa Voliboli, Malkia Strikers, sasa kupambana katika tuzo ya Kocha bora wa Mwaka, kwenye tuzo za Mwanaspoti bora wa Mwaka 2019, maarufu kama SOYA Awards.

Kocha Ouma, alimaliza mwaka 2019 kwa kishindo baada ya kuiongoza Starlets kutwaa taji la CECAFA, yaliyofanyika Dar es salaam, Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya Soka la Wanawake nchini, huku akiteleza kidogo katika kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki 2020 Tokyo Olympics.

Kama hiyo haitoshi, Ouma pia alitajwa kuwania tuzo ya Kocha bora wa Afrika kwa mwaka 2019 (CAF Awards). Aidha, kikosi chake cha Starlets kinawania tuzo hizo, katika kipengele timu bora, huku mshambuliaji wake, Jentrix Shikhangwa akitajwa kuwania kipengele cha msichana aliyebamba zaidi (Most Promising Girl).

Kwa upande Paul Bitok, baada ya kutimiza ahadi ya kuipeleka Malkia Strikers kwenye michezo ya Olimpiki, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16, sasa anakabiliwa na changamoto ya kutwaa tuzo ya Kocha bora na kumpiku mshindani wake mkuu, David Ouma.

Bitok, aliiongoza Strikers kutwaa ubingwa wa Afrika, kabla ya kuwanyorosha Cameroon (3-2), Botswana (3-0), Nigeria (3-0) na wababe Egypt (3-1) na kujikatia tiketi ya kuiwakilisha Afrika kwenye michezo hiyo itakayofanyika huko Japan, kuanzia Julai.

Bitok, pia anaringia timu yake ya Malkia kuwania tuzo hiyo itakayofanyika Ijumaa ya Januari 24, Jijini Mombasa, katika kipengele cha timu bora. Wawili hao hata hivyo, wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa Alex Alumirah (Vihiga Queens), Carey Odhiambo (Morans) na Curtis Olago (KCB RFC).