Baba Levo kutoka gerezani Peter Msechu kicheko

Muktasari:

Septemba 10, 2019 mahakama Wilaya ilimuhukumu kifungo cha mwaka mmoja na siku mbili, lakini Oktoba Mosi, 2019 Baba Levo alikata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Dar es Salaam.Nyota wa muziki wa bongo fleva, Peter Msechu ameelezea furaha yake baada ya kuwachiwa kwa rafiki yake kipenzi diwani wa Mwanga (ACT-Wazalendo), Clayton Chipando maarufu Baba Levo.

Akizungumza na www.mwanaspoti.co.tz, Msechu amesema alipata taarifa za kuachiwa Baba Levo kupitia mitandao ya kijamii na haraka akampigia simu mwanasheria wa muimbaji huyo ambaye alimthibitishia jambo jilo.

"Kwa taarifa ambazo zipo mtandaoni zinasema Baba Levo yuko huru, nilipoona hivyo niliamua kumpigia simu Mwanasheria wake na akanithibitishia kuwa yuko huru, akasema mtu akiwa huru kuna taratibu za kufuata ili atoke gerezani, hivyo taarifa za kusema anaendelea na kifungo hizo sizifahamu, nachofahamu ni yuko huru na Mwanasheria wake amethibitisha hilo," alisema Peter Msechu.

Aidha amesema amefurahishwa na tukio hilo na hasa vile alivyombambana na jambo lake na akashinda na mahakama imeona aidha alionewa au anahaki ya kutoka, sababu asingepambana kukata rufaa angeendelea kutumikia kifungo.

Agosti Mosi 2019 Baba Levo alihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela baada ya kukutwa na hatia ya kumshambulia Askari F.8350PC Msafiri Mponela.

Septemba 10, 2019 mahakama Wilaya ilimuhukumu kifungo cha mwaka mmoja na siku mbili, lakini Oktoba Mosi, 2019 Baba Levo alikata rufaa kupinga hukumu hiyo. Leo Alhamisi Novemba 21, 2019, Jaji mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mugeta amesema kifungo hicho kilikuwa batili na kuachiwa huru.