Nandy aula T-Marc awa balozi, Hadija Kopa achengua

Wednesday January 15 2020

Mwanaspoti-Nandy-T-Marc-Tanzania-balozi-Hadija Kopa-Mwanasport-Michezo blog-MICHEZO-

 

By RHOBI CHACHA

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa kizazi kipya, Nandy ameteuliwa kuwa balozi wa kampuni ya T-Marc Tanzania.

Mkurugenzi Mtendani wa T-MARC Tanzania, Tumaini Kimasa alisema leo kuwa mwanamuziki huyo anakuwa balozi wa bidhaa za taulo maalumu za kike aina ya Flowless Sanitary pads, Smiley baby diaper kwaajili ya watoto wachanga na Harmony adult diaper kwa watu wazima wenye matatizo maalumu ya kitabibu.

Kimasa alisema wameamua wamevutiwa na maendeleo ya kimuziki wa Nandy na wanaamini chini ya ubalozi wake, atafikisha kwa jamii matumizi ya bidhaa zao.

 Alisema kuwa wanatambua kazi ya sanaa katika jamii na kuamua kuwatumia wanamuziki wa Tanzania katika kunadi bidhaa zao.

Naye Nandy alisema amepata faraja kupata ubalozi huo na kuahidi kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kampuni hiyo.

“Siwezi kusema mengi, mimi ni balozi wa T-Marc Tanzania, nitafanya kazi nao kwa uadilifu mkubwa ili kuweza kuwavutia zaidi na kuendelea kupata ‘dili’nyingine,” alisema Nandi ambaye pia alifanya shoo ya nguvu katika utambulisho huo.

Advertisement

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena alipongeza jitihada za T-MARC Tanzania kwa kuja na mtizamo mpya wa uendeshaji na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo.

 “Ni chukue fursa hii kuwapongeza T-MARC kwa mfumo huu mpya wa uendeshaji ambao ni msingi wa uimara.  Katika ulimwengu wa sasa ni muhimu kwa mashirika yanayotegemea ufadhili kuangalia namna ya kupunguza utegemezi. Kwa njia hii mtaweza kuwafikia watu wengi na kwa muda wote kwa mafanikio katika jamii, "alisema.

Aidha katika uzinduzi huo msanii wa Muziki wa taarabu Khadija Kopa alialikwa kutumbuiza huku Isha Mashauzi na Johari wakiwa wageni waalikwa.

Khadija Kopa aliimba nyimbo Top in Town, Mjini Chuo kikuu na full stop ziliwainua watu waliohudhuria pamoja na Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema pamoja na wasanii Nandy, Shamsa Ford na Johari.

Advertisement