Mwamnyeto umwambie kitu kwa Yondani, Nyoni, Kagere

Monday December 9 2019

Mwanaspoti-Mwamnyeto-Tanzania-umwambie-Yondani-Nyoni-Kagere

 

UMBO alililonalo sambamba na akili na mbinu za kuwazuia washambuliaji wasumbufu vimekuwa vikimbeba, beki Bakar Mwamnyeto anayekipiga Coastal Union.
Kwa namna anavyojituma uwanjani na ule umakini wake katika kutengua mbinu za washambuliaji  imesababisha mashabiki kuamini anaweza kuwa mrithi sahihi wa beki wa kati wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars.
Yondani ndiye anatajwa kuwa beki bora kwa sasa Ligi Kuu Bara na hata timu ya Taifa kwa jinsi anavyopambana akiwa uwanjani, pia ana uzoefu mkubwa kwani ameshazichezea timu mbili kubwa Simba na Yanga huku akiwa ni mmoja wa mabeki mahiri  wanaopanda mbele kushambulia pindi anapoona mambo magumu kwa timu yake inapotafuta bao.
Wakati Yondani alipokosekana kwenye mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) dhidi ya Sudan uliofanyika Oktoba 18, mashabiki wengi hapa nchini walikuwa wana wasiwasi na kusema sasa itakuwaje.
Mashabiki walikuwa wanawaza tayari Sudan imeshaifunga Taifa Stars bao 1-0 nyumbani sasa tutaweza kweli kupindua matokeo na huku beki kisiki anayetumainiwa Yondani hayupo.
Yondani alishindwa kusafiri na timu kutokana na kuwa majeruhi ya mguu lakini kocha Etienne Ndayiragije akakuna kichwa akaona isiwe tabu ngoja kwanza amjaribu kijana mdogo kutoka Coastal Union, Bakari Nondo Mwamnyeto kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda kabla ya kuivaa Sudan.
Dogo akapiga mpira mwingi kila mtu akamsifia hivyo Watanzania kuanza kupata matumaini anaweza kucheza vizuri hata dhidi ya Sudan na ndicho kilichotokea.
Kiwango alichokionyesha Mwamnyeto katika mchezo ule dhidi ya Sudan ambao Taifa Stars ilishinda mabao 2-1 na kufuzu Chan , kilikuwa cha juu na wadau wengi wa soka kusema kuwa anaweza akaja kuwa mrithi sahihi wa Yondani pindi mkongwe huyo akiamua kutundika daruga.
Kumbe sio wadau tu wanaomuwazia hivyo ila hata yeye Mwamnyeto analijua hilo na anasema ataendelea kujituma ili kuhakikisha anakuwa kama Yondani au zaidi.

Msikieni mwenyewe
Mwamnyeto amejiaminisha kuwa ataendelea kujituma kwani anaamini yeye ni mrithi sahihi wa Yondani kwenye kikosi cha Taifa Stars.
“Yondani ni mchezaji mkongwe na bora hivyo nitajitahidi kujituma na kufuata ushauri wake ili niweze kucheza kwa ubora mkubwa kama yeye.
“Amewahi kukaa na mimi mara moja wakati tuko kambini tukijiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Chan dhidi ya Sudan ambayo tulifungwa bao 1-0 iliyofanyika Septemba 22 hapa nyumbani.
“Aliniambia dogo komaa kwani mimi ni mchezaji mzuri na ukizingatia yeye umri unaenda hivyo kama nikipambana, nikazidisha mazoezi, nitakuja kucheza bila wasiwasi na nitakuwa hata zaidi ya yeye. Hivyo naufanyia kazi ushauri wake,” anasema Mwanyeto.

Yondani, Nyoni wamkuna
Mwamnyeto anasema anawakubali sana Yondani na Erasto Nyoni kwani amekuwa shabiki yao tangu kipindi akiwa anacheza timu za madaraja ya chini.
“Yaani hao majamaa nawakubali sana, nimekuwa nawafuatilia muda mrefu wanavyocheza. Wanatumia sana akili. Mimi ni shabiki wao na siku niliyoutana nao mara ya kwanza ana kwanza sikuamini,” anasema Mwanyeto.

Msikie Yondani sasa
Yondani amekiri Mwamnyeto ni beki mzuri na umri unamruhusu kufanya makubwa zaidi hivyo azidi kupambana ili aweze kucheza kwa muda mrefu zaidi.
“Ni mchezaji mzuri na napenda anavyocheza. Nafikiri anaweza kuwa mrithi wangu pindi nikapostaafu lakini tu kama ataendelea kujituma uwanjani, kupenda mazoezi na nidhamu ya mpira.
Yondani anasema mpira hauna umri, muhimu ni mchezaji kujitunza na kujituma hiyo ndio siri iliyomsaidia hata yeye akacheza kwa kiwango bora muda mrefu.

Aukubali mziki wa Kagere
Mwamnyeto anasema hakuna mshambuliaji mgumu kumkaba kama Kagere kwani ni mchezaji mwenye nguvu na hakati tamaa kirahisi. “Nilifanikiwa kukutana na Kagere katika mechi ya timu ya Taifa dhidi ya Rwanda,yule jamaa ni balaa, kumkaba inabidi utumie akili sana.
“Nimekuwa nikimfuatilia hata kwenye ligi, mjanja sana, ana nguvu, hakati tamaa, yaani anafunga lakini bado unaona anatafuta mabao mengine  bila kuchoka,” anasema Mwnamnyeto.
 
Aziita Simba, Yanga
Beki huyo ambaye msimu huu ndio mara yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu anasema mipango yake ni kucheza timu kubwa lakini zaidi kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.
“Napenda zaidi kama nitapata timu nje ya nchi niende nikacheze kule kuliko hapa nyumbani, ingawa pia hata kama timu kubwa kama Yanga,Simba, Azam zitakuja na ofa nzuri naweza kwenda kucheza,” anasema Mwamnyeto.
Mwamnyeto anasema kabla ya kucheza Coastal Union alikuwa akicheza timu ya Majengo Fc iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mkoa wa Tanga.
“Wakati nacheza Majengo Fc ndipo Coastal waliniona nikajiunga nao mwaka 2017 na nikacheza Ligi Daraja la kwanza mpaka tukapanda kucheza Ligi Kuu msimu huu.
Mwanyeto anasema kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu Chan kitafanya vizuri kwenye Fainali hizo  ila muhimu ni kujituma na kucheza kitimu kwani anaamini wana kikosi kikali sana.

Advertisement