Msuva kuondoka Morocco mwisho wa msimu huu

Muktasari:

Msuva siku chache zilizopita alitangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu uliopita wa Difaa, alikuwa akihusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno na CD Leganés ya Hispania.

NYOTA wa Kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva anayeichezea Difaa El Jadida, amefunguka baada ya dirisha la Januari kufungwa kwa kusema wakati wake ukifika wa kwenda kucheza soka Ulaya hakuna jambo linaloweza kuwa kama kizuizi.
Katika dirisha hilo la usajili ambalo lilifungwa Ijumaa wiki iliyopita, Msuva ambaye siku chache zilizopita alitangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu uliopita wa Difaa, alikuwa akihusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno na CD Leganés ya Hispania.
Msuva alisema mazungumzo baina ya klabu yake na hizo ambazo zilikuwa zikimwitaji yaligonga mwamba kwa hiyo hana jinsi zaidi ya kusubiri hadi mwishoni mwa msimu kuona nini kitatokea.
“Mipango ya Mungu ni tofauti na wanadamu vile ambavyo tunapanga na kuwaza, nilihakikishiwa kuondoka ila imeshindikana. Mabosi wa klabu wamenitaka kuendelea kuwa mvumilivu.
“Niliwaelewa kwa sababu mbali na pesa wanatamani kuniona naenda sehemu ambayo watakuwa wakijivunia uwepo wangu, hawapendi niende sehemu ambayo naweza kupotea,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.
Msuva mwenye mabao matatu msimu huu, aliongeza kwa uwezo wa kiuchumi wa klabu mbalimbali Morocco, inaweza kuwa miongoni mwa sababu ambazo zimechangia kushindikana kuondoka Januari.
“Huku wanalipa vizuri sasa labda jamaa walitaka kunisajili kwa kiwango kidogo cha pesa.”
Difaa ambayo iliibuka na ushindi wa mabao kwenye mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Batola Pro dhidi ya Youssofie huku Msuva akicheza kwa dakika zote 90, ipo nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo.