Umemsikia bosi wa Msuva alichosema kuhusu uhamisho

Muktasari:

Vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini viliripoti kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Yanga amejiunga na SL Benfica kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini ataenda kwa mkopo Panathinaikos FC ya Ugiriki hadi mwishoni mwa msimu.

BOSI wa Difaa El Jadida, Abdelatif Moktarid ameweka wazi kile kinachoendelea kuhusu uvumi wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva ‘Msuvan27’ kujiunga na miamba ya soka ya Ureno, SL Benfica.
Vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini viliripoti kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Yanga amejiunga na SL Benfica kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini ataenda kwa mkopo Panathinaikos FC ya Ugiriki hadi mwishoni mwa msimu.
Moktarid ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu hiyo, alisema kwa sasa Msuva bado ni mchezaji wao licha ya uwepo wa ofa kadhaa kutoka mataifa mbalimbali barani Ulaya.
“Nimekuwa nikizungumza na Msuva, anaonekana kuwa na ndoto ya kucheza Ulaya, hivyo mambo yakikaa sawa hatuwezi kukaa kimya ni lazima tungetoa tamko rasmi,” alisema.
Moktarid aliongea kuwa: “Siwezi kuficha, ni kweli kuna timu zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili, ila ni muhimu kusubiri kuona nini kitatokea, siwezi kuzitaja kwa majina.”
Wapo wanaodai kuwa ishu ya Msuva kutua SL Benfica ipo mbioni kukamilika kutokana na mshambuliaji huyo kusaini mkataba wa awali tangu mwishoni mwa mwaka jana. Na ndio maana hata meneja wake ambaye alisuka dili la kwenda Difaa El Jadida akitokea Yanga, Dk Jonas Tiboroha alipata ujasiri wa kulizungumzia hilo katika vyombo mbalimbali vya habari.
Kinachotia shaka juu ya uwepo wa dili hilo ni kwamba vyombo vya habari vya Ugiriki vilikanusha taarifa kuwa Msuva ataenda Panathinaikos F.C kwa mkopo huku wakisema meneja huyo ni kama anatafuta ‘kiki’.
Kwa mujibu wa Msuva ambaye jana alikuwa safarini na Difaa ambao walikuwa wakielekea Agadir umbali wa saa mbili kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Morocco ambao watacheza Jumanne dhidi ya Hassania Agadir, alisema taarifa njema zipo njiani.