Mourinho kuivunja rekodi tamu ya Liverpool leo

Saturday January 11 2020

Mwanaspoti-Mourinho-tanzania-England-kuivunja-Liverpool-EPL-Ole-Pep leo

 

LONDON, ENGLAND. ZAMU ya nani leo? Nani atapigwa? Jose Mourinho anakipiga na Jurgen Klopp. Lakini, yule Robbie Savage, staa wa zamani kwenye Ligi Kuu England amesema Mourinho atakula nyingi tu.
Ni hivi, makocha hao wataziongoza timu zao Tottenham Hotspur na Liverpool kumenyana kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakapigwa leo Jumamosi. Mechi hiyo inatajwa kuwa mtihani mzito kwa Liverpool inayotaka kuendelea kugawa dozi kwenye ligi hiyo ili kubeba taji kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka 30.
Mourinho na Spurs yake atahitaji kushinda ili kusogea kwenye Top Four inayotoa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Klopp kikosi chake kipo kwenye mwendo wa kutisha kikiwa na dhamira moja ya kuelekea kuvunja rekodi ya Arsenal ya kucheza msimu bila ya kupoteza.
Lakini, mechi zote zitakazopigwa leo kwenye Ligi Kuu England, Savage ameandika utabiri wake na kusema kipute hicho kitakachopigwa London, Spurs itakumbana na kipigo kisichopungua mabao matatu.
Mechi nyingine kali ya kutazamwa itakuwa huko London, Selhurst Park, wakati Crystal Palace ya Wilfried Zaha itakapoikaribisha Arsenal ya Mikel Arteta. Baada ya kuichapa Manchester United kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu England, Arsenal inaonekana kuwa kwenye morali wa kwenda kufanya kweli nyumbani kwa Palace.
Lakini Savage ametia utabiri wake kwenye mechi hiyo kwamba itamalizika kwa sare ya kufungana. Mechi hiyo itapigwa mchana kweupe. Savage ameitazama Spurs, kisha akaitazama Liverpool na kuona hakuna namna Mourinho atakwepa kipigo. Rekodi pia zinambeba Klopp, ambapo kwenye mechi 10 zilizopita alizocheza dhidi ya Mourinho, Mjerumani huyo amepoteza mechi mbili tu, huku safari hii Mourinho akienda kumkabili mpinzani wake huyo akiwa na majeraha kibao kwenye kikosi chake akiwamo straika wake namba moja, Harry Kane.
Manchester United nayo ina shughuli mbele ya Norwich City. Tangu mwaka huu, 2020 uingie, kikosi hicho cha Ole Gunnar Solskjaer hakijashinda, huku kikifanikiwa kupata bao moja tu katika kipigo cha 3-1 kutoka kwa Manchester City kwenye Kombe la Ligi. Sasa itashuka tena uwanjani Old Trafford kuikabili Norwich City ya straika matata, Teemu Pukki. Savage anaitabiria Man United kushinda mechi hiyo kwa zaidi ya mabao mawili.
Man United ipo kwenye harakati za kuifukuzia Chelsea kwenye Top Four, ambapo timu hizo zimetofautiana pointi tano, huku The Blues chini ya kocha wake, Frank Lampard watakuwa nyumbani Stamford Bridge kuikabili Burnley.
Savage ameipa ushindi Chelsea kwenye mechi hiyo kwa zaidi ya mabao mawili.
Kuhusu Man United, Savage anaamini itashinda tu licha ya kuwa na kiwango kibovu na hilo linatokana na wapinzani wao, Norwich City kutoshinda mechi yoyote kati ya nane za mwisho walizocheza kwenye ligi na wataendelea kupokea kichapo wikiendi hii.
Arteta ameichapa Man United, lakini Savage haoni kama ataiweza Palace katika mchezo huo wa leo, licha ya kwamba The Gunners kwa sasa wameonekana kuwa kwenye moto wakiwachapa pia Leeds United katika raundi ya tatu ya Kombe la FA.
Mechi nyingine za michuyano hiyo itashuhudia Brighton ikisafiri kuifuata Everton, huku Southampton ikiwa na kazi ya kuzuia wasikumbwe na aibu ya raundi ya kwanza ilipochapwa 9-0 na Leicester City itakapokwenda kucheza King Power, huku Wolves ikiwa na kibarua cha kuikabili Newcastle United.
Kesho Jumapili, Bournemouth itakuwa nyumbani kuikabili Watford wakati mabingwa watetezi Manchester City watakwenda jino kwa jino na Aston Villa.
Utabiri wa Savage ni kwamba Kocha Pep Guardiola na chama lake la Man City watakwenda kushinda tu kirahisi mchezo huo utakaofanyika Villa Park - tena kuanzia mabao mawili na kuendelea.
Anachokiaminni Savage pia, Everton ya Carlo Ancelotti itajipigia tu Brighton huko Goodison Park, huku Brendan Rodgers na Leicester City yake, ataichapa bila ya shida Southampton huku akisema Wolves itaibuka na ushindi finyu mbele ya Newcastle United na Bournemouth hawataiweza Watford nyumbani.
Liverpool inayoongoza ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 58 katika mechi 20 ilizocheza, ikiwa ni tofauti ya pointi 13 dhidi ya timu inayowafuatia kwenye msimamo wa Ligi Kuu England inaaminiwa itashinda. Je, Mourinho ataweza kuizuia?

Advertisement