Mkwasa ampiku Sven wa Simba SC, Kahata mchezaji bora

Tuesday January 7 2020

Mwanaspoti-Mkwasa-Tanzania-Yanga-Sven-Simba SC, Kahata-Kenya-mchezaji bora

 

By THOMAS NG'ITU

Dar es Salaam.Kiungo mshambuliaji wa Simba SC ya Dar es Salaam, Francis Kahata amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Desemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2019/20, huku Boniface Mkwasa wa Yanga akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo. 

Mkwasa na Kahata walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao katika uchambuzi na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 

Desemba 2019, Simba ilicheza michezo mitatu, ikishinda yote, iliifunga Lipuli mabao 4-0, ikaifunga KMC mabao 2-0 na pia ikaifunga Ndanda mabao 2-0, huku Kahata akiwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Simba kwa mwezi huo na alikuwa katika kiwango bora ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi ya mwisho moja. 

Kahata aliwashinda Hassan Dilunga wa Simba na Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union alioingia nao fainali, ambapo Dilunga naye alikuwa sehemu ya mafanikio hayo ya Simba akifunga mabao mawili na kutoa pasi ya mwisho moja, wakati Mwamnyeto alitoa mchango kwa Coastal Union iliyocheza michezo miwili na kushinda yote, ikiifunga Azam FC bao 1-0, kisha ikaifunga Mbeya City mabao 2-0. 

Kwa upande wa Mkwasa aliwashinda Juma Mgunda wa Coastal na Sven Vandenbroeck wa Simba, ambapo Mkwasa aliiongoza timu yake katika michezo minne, akishinda miwili na kutoka sare moja na kupanda kutoka nafasi ya tisa hadi ya pili katika msimamo.

Yanga iliifunga Prisons bao 1-0 na ikashinda idadi kama hiyo dhidi ya Biashara United na kutoka sare ya bao 1-1 na KMC na ilitoka 0-0 na Mbeya City. 

Advertisement

Kocha Vandenbroeck aliiongoza Simba kushinda michezo mitatu, iliifunga Lipuli mabao 4-0, ikaifunga KMC mabao 2-0 na pia ikaifunga Ndanda mabao 2-0 na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi, huku Mgunda akiiongoza Coastal kushinda michezo miwili, iliifunga Azam FC bao 1-0, kisha ikaifunga Mbeya City mabao 2-0 na kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya tano.

Advertisement