Kufyekwa Aussems kumetikisa kinoma Tanzania

Monday December 2 2019

Mwanaspoti-Kufyekwa-Aussems-kumetikisa-kinoma-Tanzania-Simba Sc-Yanga-Zahera

 

By ELIYA SOLOMON

Dar es Salaam. UNASIKIA buana, unaambiwa eti kama Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ angepata nafasi ya kuongea na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji angemshauri kuwatimua pia na viongozi walioitumikia Simba kwa zaidi ya miaka 15.
Unajua kwanini, Julio kasema hivyo? Hii ni baada ya kushtushwa na uamuzi wa kumfukuza kazi Kocha Patrick Aussems akidai timuatimua ya makocha inachangiwa na viongozi ving’ang’anizi ndani ya Simba.
Aussems amefutwa kazi kwa sababu kadhaa akifuata nyayo za Mwinyi Zahera, ambaye naye amefutwa kazi hivi karibuni pale Yanga.
Aussems inaelezwa alitimuliwa kitambo, lakini uongozi uliokuwa unaweka sawa baadhi ya mambo hasa ya kisheria ili kukwepa kuingia kwenye mtego wa kulipa fidia nene.
Kwanza, aliitwa kujieleza kutokana na madai ya kuondoka kituo cha kazi na kwenda Afrika Kusini bila kibali na kushindwa kusimamia suala zima la nidhamu. Sasa unaambiwa kutimuliwa kwa Aussems hakujamshtua Julio pekee, bali wadau, makocha na hata wachezaji waliowahi kunolewa na Aussems, lakini Julio alisema; “Amefeli msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini sio kwa sababu Simba ilikuwa mbovu, alikuwa na uhitaji wa kuendelea kufanya kazi na wachezaji wake aliopata nao mafanikio msimu uliopita.
Nadhani tunakumbuka kilichotokea, viongozi hawakuona umuhimu wa kuwazuia Okwi na Kotei.
“Huwezi kujenga kwa kubomoa, nilitegemea kuona yakifanyika maboresho ila sio kwa kuondoka kwa wachezaji muhimu kuletewa hao Wabrazil kwani, bado amejitahidi kuifanya Simba kufanya vizuri katika Ligi.
Nasemaje kwa Simba tatizo lipo kwa viongozi na wala sio Aussems.”
Alisema itakuwa vyema yakitoka maamuzi pia ya kutimuliwa viongozi waliokaa Simba kwa zaidi ya miaka 15, inawezekana ndio sababu ya kutengeneza fitna za kuondolewa makocha ndani ya kipindi kifupi huku zikitolewa sababu zisizo na msingi kwa manufaa yao binafsi.
Naye nyota na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Abdallah Kibadeni, alisema kufikia mafanikio malengo ya kufanya vizuri karibu katika kila msimu katika mashindano ya kimataifa kuna baadhi ya mambo yanatakiwa kuwekwa sawa.
“Sio vyema kufukuza hovyo makocha, ni muhimu klabu kuwa na utaratibu wa  watakaa na makocha kwa muda mrefu, ukifukuza kocha ina maana wanakuja mwingine kuanza upya, hatujui itachukua muda gani kutengeneza muunganiko kwa wachezaji kulingana na mbinu zake,” alisema.
Kiungo wa zamani wa  Yanga, Sekilojo Chambua alisema umekuwa utamaduni kwa Simba na Yanga kutimua makocha ndani ya kipindi kifupi.
“Ishu ya Simba kumfukuza Aussems labla kuwe na sababu nyingine ambazo zimefichwa lakini sio kwa sababu ya mwenendo wa klabu, siamini kama Simba ina mwenendo mbaya, wanaongoza Ligi, kama kuna mengine wangekaa chini kuyamaliza, ni ngumu kupata aina ya kocha kama Aussems.”

MSIKIE HANS NAYE
Kocha wa zamani wa Yanga na Azam, Hans Pluijm alisema aliwahi kumweleza Aussems kama rafiki yake juu ya  maisha ya soka la Tanzania hasa kwa Simba na Yanga.
“Tulikuwa tukiongea, binafsi ni kati ya makocha niliyemkubali. Nakumbuka kuna siku nilimweleza, kuwa kuna presha kubwa kuzifundisha Simba na Yanga, zinafanana hasa kwa aina ya uongozi na hata mashabiki,” alisema.
Kwa upande wa mbinu, Pluijm alisema Aussems ni kati ya makocha bora waliokuwa wakimsumbua kipindi akiwa Azam na  katika mchezo wa mwisho kukutana naye Februari 23 mwaka huu, alipoteza kwa mabao 3-1 kabla ya siku iliyofuata kutimuliwa, Azam.
Akisimulia kisa chake kilichomfanya kuondolewa Yanga, alisema ilikuwa miaka miwili iliyopita alipopokea barua, akiwa katika majukumu ya ukurugenzi wa ufundi baada ya kuondolewa katika ukocha kufuatia ujio wa Mzambia George Lwandamina.
“Nilikuwa na utayari wa kufanya kazi Yanga hata bure, lakini nilielezwa katika barua hiyo kuwa uongozi wa juu umeamua kusitisha mkataba kutokana na ukata wa fedha. Nimekuwa Yanga kwa mapenzi makubwa na nilikuwa tayari kuhakikisha tunaendelea kujenga mifumo bora ya kuifanya kuwa tishio Afrika,” alisema kocha huyo, ambaye kwa sasa ameweka makazi yake nchini Ghana.

MAPRO WA KIGENI WAFUNGUKA
Nyota wa kigeni waliopo Simba, Cletous Chama na Meddie Kagere na aliyekuwa staa wa klabu hiyo msimu uliopita, Emmanuel Okwi wametoa hisia zao juu ya kuondoka kwa Aussems.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa Twitter, Chama aliposti akimshukuru kocha huyo, aliyemwachia kumbukumbu ya msimu uliopita na kubeba pamoja ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku.
Kagere aliyekuwa Mfungaji Bora msimu uliopita aliposti, “Ilikuwa poa kufanya kazi na wewe (Aussems), nakutakia kila la kheri katika maisha mpya.”
Okwi, ambaye kwa sasa anaichezea Al Ittihad, alisema ni taarifa ya kusikitisha ila akamtakia kila la kheri.

SHEVA  YUMO
Mshambuliaji wa Simba, Miraj Athuman alisema atamkumbuka Aussems kama kocha aliyemwamini na kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza licha ya kutokea timu ndogo.
“Aliangalia zaidi kiwango changu na sikutaka kumwangusha, nitaendeleza mazuri aliyonifundisha, namtakia kila la kheri,” alisema mchezaji huyo mwenye mabao sita Ligi Kuu Bara.
Aussems anaondoka Simba akiwa ameiongoza kwa siku 498 katika mechi 48 za Ligi Kuu Bara, sambamba na michezo mingine 14 ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019 na 2019-2020 na kuacha alama ya kufika robo fainali. Pia, amebeba  mataji matatu, moja ya Ligi Kuu na Ngao mara mbili.

Advertisement