Kilimanjaro Stars yaiingia 4-4-2 kwa Zanzibar

Muktasari:

Mara ya mwisho kwa Kilimanjaro Stars kutwaa ubingwa wa mashindano ya Chalenji ilikuwa ni 2010 yalipofanyika jijini Dar es Salaam.

Kampala, Uganda. Kocha wa timu Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', Juma Mgunda amefanya mabadiliko manne katika kikosi chake kitakachoiva na Zanzibar 'Zanzibar Heroes' kwenye Uwanja wa KCCA, Kampala.

Wachezaji wanne walioanza katika mchezo wa kwanza wa mashindano haya ya Chalenji dhidi ya Kenya 'Harambee Stars' ambao Kilimanjaro Stars ilifungwa bao 1-0, wamerudishwa benchi ambao ni Mohamed Hussein, Lucas Kikoti, Paul Nonga na Cleoface Mkandala.

Badala yao Mgunda ameamua kuwaanzisha Gadiel Michael, Hassan Dilunga, Eliuter Mpepo na Ditram Nchimbi.

Mabadiliko makubwa yamefanyika katika safu ya ushambuliaji ambapo wachezaji watatu kati ya wanne walioanza mechi iliyopita leo wataanzia benchi huku kwenye ulinzi kukiwa na badiliko moja tu la upande wa beki ya kushoto.

Tofauti na mechi iliyopita ambayo Stars ilianza na mfumo wa 4-5-1, leo itaanza na ule wa 4-4-2 ikionekana imepanga zaidi kushambulia na kujenga mashambulizi yake kupitia pembeni.

Kikosi hicho kinawajumuisha Aishi Manula, Mwaita Gereza, Gadiel Michael, Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Ditram Nchimbi, Eliuter Mpepo na Miraji Athumani