Kilimanjaro Stars, Zanzibar Heroes undugu tupa kule leo

Muktasari:

Kili Stars inahitaji japo sare kufufua matumaini ya kubaki mashindanoni na ni lazima ishinde mechi yao ya mwisho dhidi ya Sudan Jumamosi ili kuona kama itaenda nusu fainali.

HATIMA ya timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kwenye mashindano ya Chalenji hapa Uganda itaamuliwa leo katika mechi yao ya pili ya Kundi B dhidi ya ndugu zao, Zanzibar Heroes kwenye Uwanja wa KCCA.
Kipigo mikononi mwa Zanzibar, kitakuwa ni kama hitimisho la ushiriki wa Kili Stars katika mashindano hayo baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Kenya juzi Jumapili.
Kili Stars inahitaji japo sare kufufua matumaini ya kubaki mashindanoni na ni lazima ishinde mechi yao ya mwisho dhidi ya Sudan Jumamosi ili kuona kama itaenda nusu fainali.
Zanzibar ambayo ina pointi moja baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Sudan katika mechi ya ufunguzi, inahitaji kushinda pia leo ili kuepuka presha ya kuwakabili mabingwa watetezi Kenya katika mechi yao ya mwisho Jumamosi.
 Mechi ya mwisho kati ya Zanzibar na Kenya Jumamosi itakumbushia fainali ya mashindano yaliyopita ya Chalenji yaliyofanyika nchini Kenya 2017 ambayo wenyeji walishinda kwa penalti 3-2 na kutwaa taji lao la 21 la michuano hiyo mikongwe zaidi Afrika inayohusisha mataifa iliyoanzishwa mwaka 1926.
Ni hitajio ambalo benchi la ufundi na kikosi cha Stars wanafahamu kabla hata ya mchezo kama ilivyothibitishwa na kocha Juma Mgunda. “Hii ni mechi ambayo kwa namna yoyote tunahitajika kupata ushindi ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kucheza nusu fainali na si vinginevyo. Tunalifahamu hilo na tutafanya kila liwezekanalo tushinde,” alisema Mgunda.
Timu mbili kutoka katika kila kundi zitaingia nusu fainali ya mashindano hayo ambayo mwaka huu yanashirikisha mataifa tisa tu baada ya wanachama wengine wa Cecafa kujitoa kutokana na ukata.
Zanzibar licha ya kulitwaa taji la Chalenji mara moja tu tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1949, inajivunia kucheza katika ardhi ambayo walibeba kombe hilo mwaka 1995 baada ya kuifunga Uganda B’ bao 1-0 katika mechi ya fainali.
Kocha wa Heroes, Hemed Morocco amekiri ugumu unaoletwa kwenye hesabu ikiwa watapoteza mechi ya leo na kuahidi timu yake itapambana kufa au kupona ili iweze kupata ushindi.
“Wote tumeanza vibaya, ingawa sisi tumetoka sare lakini hilo halitupi nafuu kwani tukipoteza dhidi ya Kilimanjaro Stars tutazidi kujiweka katika mazingira magumu kwenye mchezo wa mwisho,” alisema.
Ndani ya uwanja ni mechi inayoonekana itatawaliwa na ubabe zaidi hasa katika safu ya kiungo ambayo kila timu imeonyesha kabla ya kukutana kwao, lakini pia kufahamiana vyema kwa wachezaji wa timu zote mbili.
Timu hizo zinapendelea zaidi kumiliki mpira hasa katikati ya uwanja na haikushangaza kuona kila upande ukitumia idadi kubwa ya viungo katika mechi zilizopita ambapo zilitumia wachezaji watano wanaocheza katika eneo hilo.
Lakini kila upande ukionekana kupatazama zaidi katikati mwa uwanja ambako inaonekana ndiko zina uimara, bado zinakabiliwa na changamoto ya udhaifu wa safu za ulinzi kufanya makosa ya mara kwa mara na kukosa utulivu pindi zinapokutana na presha ya washambuliaji wa timu pinzani.
Lakini pia bado timu zote mbili zimekuwa na changamoto ya kushindwa kutumia nafasi ambazo zimekuwa zikitengeneza na hivyo kushindwa kufunga mabao yanayoweza kuzibeba.
Zanzibar inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na pigo la kumkosa mshambuliaji wake Ibrahim Ilika ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyopita na pengo lake huenda likazibwa na Kassim Khamis.
Hakuna mabadiliko mengine yanayoonekana yatakuwepo kwa Zanzibar ukiondoa hilo na nyota wengine 10 waliocheza mechi ya kwanza dhidi ya Sudan wanaoonekana wataanza kikosini.
Kilimanjaro Stars, kuna mabadiliko kadhaa ambayo yanaweza kufanyika kikosini ambapo Juma Abdul, Eliuter Mpepo, Gadiel Michael na Ditram Nchimbi wanaweza kuanza kuchukua nafasi za Paul Nonga, Lucas Kikoti, Mwaita Gereza na Mohamed Hussein.
Mchezo huo utachezwa mnamo saa 10 jioni katika Uwanja wa KCCA uliopo Lugogo, Kampala na utatanguliwa na mechi kati ya Kenya na Sudan.
Kikosi tarajiwa cha Kili Stars leo: Aishi Manula, Juma Abdul, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude, Miraji Athuman, Mzamiru Yassin, Ditram Nchimbi, Eliuter Mpepo na Cleoface Mkandala.
Zanzibar: Ali Suleiman, Mohamed Ame, Haji Mwinyi, Ali Ali, Abdallah Kheri, Abdulaziz Makame, Awesu Awesu, Mudathir Yahya, Kassim Khamis, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mohamed Issah ‘Banka’.