Kigogo Yanga ataja kinachoizamisha, amtaja Kocha Zahera

Muktasari:

Yanga kuna mambo yanayoifanya izame na lazima hatua za haraka zichukuliwe. Mosi ni kwamba hakuna ubishi kuwa, Kocha Mwinyi Zahera na msaidizi wake Noel Mwandila hawana uwezo hata wa kuwa makocha wasaidizi wa Yanga na wanapaswa kuachishwa haraka

ACHANA na matokeo ya mechi ya marudiano ya Yanga dhidi ya wenyeji wao Pyramids iliyochezwa usiku wa jana Jumapili mjini Cairo Misri, ukweli ni kwamba ndani ya Yanga kuna sintofahamu, japo viongozi wa juu wa klabu wamekuwa wakikwepa kuanika ukweli.
Suala la kushindwa kupatikana kwa Katibu Mkuu mpya tangu alipojiuzulu, Boniface Mkwasa, kuchemsha kwa timu ikiwa imefanya usajili wa kishindo na kushindwa kulipwa kwa madeni ya wachezaji ambao baadhi wameamua kukimbilia kushtaki kwenye Shirikisho la Soka (TFF) ni mfano tu.
Pia kuwapo kwa shinikizo kutoka kwa wanachama na mashabiki wa Yanga wanaotaka Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera atimuliwe kutokana na kuonekana kushindwa kuiongoza timu, ni kati ya mambo ambayo yamekuwa yakidaiwa kufukuta Jangwani, lakini hayaelezwi bayana.
Hata hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Dk. Athuman Kihamia ameamua kuvunja ukimya na kuanika mambo 10 yanayoweza kuiporomosha na kuizamisha timu yao kwa msimu huu alipozungumza na Mwanaspoti. Ebu tiririka naye.
Kihamia aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), anasema hali ya mambo ndani ya Yanga sio shwari na ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa kutibu tatizo, klabu hiyo inaweza kujikuta inafanya vibaya zaidi katika ligi na mashindano mengine.
Kihamia anafichua kwa kusema; “Najua wapo watu watasema kwanini nisingezungumzia haya ndani ya uongozi, lakini jibu ni rahisi tu kwamba utekelezaji wa maazimio hauko sawa. Msemakweli ni mpenzi wa Mungu hata kama ukweli huo uwe umekuja kwa kuchelewa.”

HAKUNA KOCHA
“Ila Yanga kuna mambo yanayoifanya izame na lazima hatua za haraka zichukuliwe. Mosi ni kwamba hakuna ubishi kuwa, Kocha Mwinyi Zahera na msaidizi wake Noel Mwandila hawana uwezo hata wa kuwa makocha wasaidizi wa Yanga na wanapaswa kuachishwa haraka,” anasema.
“Kilichosababisha msimu uliopita waonekane wa maana ni kule kujitolea kuhamasisha wanachama wachangie timu yao na kukosekana kwa akidi ya uongozi,” anaongeza.
Yanga ilimuajiri Zahera kipindi cha uongozi uliopita baada ya Mzambia George Lwandamina kutimka kikosini klutokana na hali mbaya ya kiuchumi iliyokuwa nayo klabu hiyo na kumuacha Mwandila aliyekuja naye, ambaye amebaki kumsaidia Zahera kwa muda wote mpaka sasa.

ISHU ZA USAJILI
Kwenye dirisha kuu la usajili, nyota kadhaa wa Yanga walitimika kikosini kwa sababu tofauti na Kihamia anasema ni sababu ya timu yao kuyumba na kufafanua; “Lakini pili, kocha Zahera amewaondosha wachezaji muhimu wanaomuambia ukweli kina Ibrahim Ajibu, Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Thabani Kamusoko, Haji Mwinyi na kadhalika huku akiwachonganisha kwa Wanayanga kupitia vyombo vya habari.”
Dk Kihamia anasema licha ya klabu hiyo kutenga fungu la kutosha kwa ajili ya kuimarisha kikosi, aina ya usajili uliofanyika haukuwa mzuri na pia kumekuwa hakuna maelewano mazuri baina ya viongozi.
Kwa msimu huu chini ya Zahera, Yanga imesajili karibu wachezaji 13 wakiwamo tisa wa kigeni; Issa Bigirimana, Patrick Sibomana, Farouk Shikhalo, Lamine Moro, Mustafa Suleman, David Molinga, Juma Balinya, Maybin Kalengo na Sadney Urikhob. Wengi wao wanacheza namba zinazofanana huku baadhi ya namba zikiwa na upungufu mkubwa kama za ulinzi za pembeni, wingi na mshambuliaji wa kati.

KAMATI PASUA KICHWA
Dk Kihamia pia amegusia baadhi ya kamati zilizopo Yanga ni pasua kichwa kwa kufunguka;
“Kamati ya mashindano haina uzoefu na haisikilizi ushauri wa wanachama wenye uzoefu, kiufupi imeshindwa kabisa kwenda na kasi ya soka la sasa hivi,” anasema na kuongeza;
“Hakukuwa na sababu yoyote ya kuwaacha nje ya kamati kwa wakati mmoja wanachama wenye uzoefu wa usajili na mashindano wakiwemo Seif Magari, Abdallah Bin Kleib, Lucas Mashauri, Samuel Lukumay, Hussein Nyika, Isaac Chanji na wengineo. Simaanishi kwamba wangechukuliwa wote kwa mpigo isipokuwa hata baadhi yao kutokana na uzoefu na kujitolea kwao na sasa pengo lao lipo wazi sana.”

USIRI MWINGI
Kamati ya usajili haikutimiza wajibu wake na ikamtegemea kocha kwa asilimia 100. Matokeo yake ameleta wachezaji wa kigeni ambao wengi wao hawana viwango vya kuchezea klabu kubwa kama Yanga huku zikitumika fedha nyingi kwenye usajili huo usiokuwa na tija na kuiongezea klabu mzigo wa madeni,” alisema DK. Kihamia.
Kihamia alisema katika hali ya kushangaza kumekuwa hakuna uwazi kwenye baadhi ya mambo ikiwemo kuuzwa kwa mshambuliaji Heritier Makambo.
“Hata suala la kuuzwa Makambo halipo bayana na hakukuwa na uamuzi wa mwisho, badala yake kocha kamalizana na Horoya huku uongozi ukipigwa na butwaa,” anasema.

HAKUNA UMOJA
Uongozi wa juu wa Yanga hauna umoja wa kweli, ndio maana maazimio ni mengi ila hakuna utekelezaji wake. Hii imechangiwa sana na kukosekana kwa sekretarieti kwa kuwa kila linaloamuliwa na Kamati ya Utendaji, badala ya kutekelezwa kunakuwa na kamati ndogo ya utendaji au wajumbe wachache au na mchanganyiko wa watu wa nje ya kamati ambao wanatoa maamuzi ndani ya maamuzi.”