Kibabage atamani namba ya kudumu Taifa Stars

Muktasari:

Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na timu za taifa za vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20 kwa sasa yupo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kinachoshiriki mashindano ya Chalenji hapa nchini Uganda.

BEKI Nickson Kibabage anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Difaa el Jadida ya Morocco ameelezea matumaini yake ya kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na timu za taifa za vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20 kwa sasa yupo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kinachoshiriki mashindano ya Chalenji hapa nchini Uganda.
Kibabage alisema anaamini huu ni wakati sahihi kwake kuanza kupata nafasi katika kikosi cha Stars.
“Kiukweli nina kiu ya kuichezea Taifa Stars na natamani kupata nafasi ya kuteuliwa kwa sababu ni ndoto ya kila mchezaji kuitumikia timu ya taifa kwani ni heshima kubwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, mwishowe, suala la kuitwa na kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza linabakia kuwa ni uamuzi wa benchi la ufundi hivyo kama wakiona nastahili au sistahili nitapokea huo uamuzi,” alisema Kibabage.
Beki huyo alijiunga na Jadida mwaka jana baada ya klabu hiyo ya Morocco kukoshwa na kiwango bora alichokionyesha katika mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Afcon U17) yakiyofanyika Gabon mwaka 2017.
Katika mashindano hayo, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ iliishia katika hatua ya makundi ikishika nafasi ya tatu.