Ukimya watanda Bandarini!

Muktasari:

Jambo hilo halikuweza kuthibitishwa kutokana na kukosekana kwa Mwalala na Oburu ambao wangelikuwa na maoni. Haikufahamika pia kama timu hiyo ilifanya mazoezi nje ya uwanja wao wa Mbaraki ama ilikuwa ikifanya nje ikiwemo fuo za bahari.

MOMBASA, Kenya. KUMEKUWA na ukimya wa hali ya juu wa maofisa wa Bandari FC kuhusu kurudi kiwanjani kwa timu hiyo inayoanza kampeni yake ya mechi zao hapo Jumamosi itakapokabiliana na Nzoia Sugar katika uwanja wa Mbaraki Sports Club.
Kocha Mkuu Bernard Mwalala pamoja na meneja wa timu Wilson Oburu hawakupatikana kwenye simu zao, ambapo fununu zinaambia Mwanaspoti kuwa wako na harakati ya kutaka kuhakikisha timu hiyo imepata pointi zote tatu kwa mechi hiyo ya nyumbani.
Timu hiyo ilirudi kiwanjani kwa mazoezi wiki moja na nusu iliyopita, lakini program ya mipango yao ya mazoezi haikupatikana, hivyo inaonyesha kuna mipango ya ‘kisiri’ ya kutaka kuingia kiwanjani Jumamosi na kishindo. Tetesi ambazo hazikuweza kuthibitishwa zinafahamisha Mwanaspoti kuwa kuna watu wa timu ambazo zinatarajia kupambana na Bandari wamekuwa wakionekana kiwanjani kwa minajili ya kusoma mbinu za timu hiyo ya Pwani ili iweze kupanga itakapokabiliana.
Lakini jambo hilo halikuweza kuthibitishwa kutokana na kukosekana kwa Mwalala na Oburu ambao wangelikuwa na maoni. Haikufahamika pia kama timu hiyo ilifanya mazoezi nje ya uwanja wao wa Mbaraki ama ilikuwa ikifanya nje ikiwemo fuo za bahari.
Hata hivyo, mashabiki wa timu hiyo wanasema wana mategemeo makubwa ya timu yao hiyo9 kufanya vizuri kwenye mechi zao kutokana na wachezaji wake kupata muda wa kutosha wa mapumziko.“Tuna imani kubwa ya Bandari yetu kurfanya vizuri kwenye mechi zao zijazo sababu wanasoka wetu wamepumzika vya kutosha na sababu ya uchovu haiko tena,” akasema shabiki sugu wa timu hiyo, Rajabu Mohamed wa huko Msambweni.