Mashabiki watakiwa kufurika Mbaraki kuishuhudia Bandari v Nzoia Sugar FC

Muktasari:

Bandari FC ni timu pekee ya jimbo la Pwani inayoshiriki kwenye ligi kuu hali  timu mbili nyingine Coast Stima na Modern Coast Rangers FC ziko kwenye Supaligi ya Taifa ambayo mshindi wake anafuzu kupanda ngazi hadi Ligi Kuu.

MOMBASA. MASHABIKI wa soka wa jimbo la Pwani wanatakiwa kujitokeza kwa wingi uwanjani Mbaraki Sports Club hapo Jumamosi timu yao ya Bandari FC itakapokabiliana na Nzoia Sugar FC kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally aliyesema kuna umuhimu timu hiyo kupata ushindi ili ipate kurudia hali yake nzuri ya kupata ushindi kwenye mechi zao zilizobakia.
Baghazally alisema ni muhimu kwa mashabiki wa soka wa Pwani kujitokeza kwa wingi kwa ajaili ya kuwapa motisha wachezaji washinde baada ya kupoteza mechi kadhaa hapo awali.

“Wanasoka wamepumzika vya kutosha, sasa ni muhimu kurudia hali nzuri tuliyokuwa nayo hapo awali,” akasema.
Naye aliyekuwa mchezaji wa Black Panther FC, Mohamed Ali Obore aliwataka wachezaji wa Bandari wacheze kwa ari na moyo wa kuipenda timu ili iweze kufanya vizuri kama mwaka uliopita ambapo timu ilifanikiwa kushinda taji la SportPesa Shield.
“Nina imani kubwa kuwa kocha Bernard Mwalala atawaongoza vijana wetu kwenye ufanisi ili timu yetu hiyo ipate tena fursa ya kutuwakilisha kwenye dimba la Caf Confederation Cup,” akasema Obora.
Alisema matokeo mabaya yalipatikana karibu na mwisho wa Mwaka jana ni kutokana na sababu ya wachezaji kuonyesha uchovu baada ya kucheza mechi nyingi za ligi kuu na zile za barani Afrika.
Bandari FC ni timu pekee ya jimbo la Pwani inayoshiriki kwenye ligi kuu hali  timu mbili nyingine Coast Stima na Modern Coast Rangers FC ziko kwenye Supaligi ya Taifa ambayo mshindi wake anafuzu kupanda ngazi hadi Ligi Kuu.