Afriyie: Gor Mahia ikipata ganji, Afrika Itatii!!

Muktasari:

Kuondoka kwa Francis Afriyie, aliyesajili kandarasi ya miaka miwili na nusu katika klabu ya Township Rollers ya Botswana pamoja na mwenzake wa Ivory Coast, Gnamien Yikpe aliyekimbilia Yanga SC ya Tanzania, ilikuwa ni pigo kubwa kwa Gor Mahia, wanaosaka kuweka rekodi ya kutwaa ligi ya KPL mara nne mtawalia.

Nairobi. Siku chache baada ya kuigura kambi ya jeshi ya kijani ya Gor Mahia, Mshambuliaji kutoka Ghana, Francis Afriyie, amepasua mbarika na kusema kuwa, mabingwa hap mara 18 wakipata ganji, watakuwa klabu moto kubwa Afrika.

Afriyie, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, kwa lengo la kuziba nafasi iliyowachwa na Jacques Tuyisenge aliyeondoka, aliigura K’Ogalo kutokana na tatizo la msoto linalokabili mabingwa hao watetezi wa KPL, pamoja na vilabu vingine vya KPL, hasa baada ya SportPesa kukanyaga kubwa kubwa.

Kuondoka kwa Straika huyo, pamoja na mwenzake wa Ivory Coast, Gnamien Yikpe aliyekimbilia Yanga SC ya Tanzania, ilikuwa ni pigo kubwa kwa Gor Mahia, wanaosaka kuweka rekodi ya kutwaa ligi ya KPL mara nne mtawalia. Francis Afriyie alisajili mkataba wa miaka miwili na nusu, kuichezea Township Rollers ya Botswana.

Kuhusu sababu za kuitosa Kogalo, Afriyie (25), alisema kilichomuondoa ni msoto unaokabili klabu hiyo, huku akisisitiza kwamba kama sio sababu hiyo, asingeondoka kwa sababu Gor Mahia ni klabu kubwa na kama ingekuwa na ganji za kutosha, Afrika nzima ingejua haijui.

"Nilijua mambo yangekuwa tofauti. Lakini haikuwa hivyo, nilitamani sana kuendelea kuichezea Gor, siku nilizokaa hapo nilienjoy sana, hata hivyo kusota kwao kulinikimbiza. Hii ni klabu kubwa sana. Mashabiki wao wanatisha sana na kama wangekuwa na pesa, Afrika ingejua haijui,” alisema Afriyie.

Gor Mahia, inayoshuka dimbani kesho, ugani Bukhungu kucheza mechi ya KPL, dhidi ya Kakamega Homeboyz, kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye jedwali, ikiwa na pointi 32. Mechi ya kesho ni ngumu sana, kwani mara ya mwisho timu hizi kukutana, Gor ilishinda 3-0 na sasa Homeboyz inataka kulipiza kisasi.