Kalamu ya Samatta inamwaga wino ila kina nani wanasoma?

Muktasari:

Kalamu hii, inapoendelea kumwaga wino. Macho yako yanapoendelea kusoma makala haya, elewa kwamba, mafanikio ya nahodha huyu msaidizi wa KRC Genk na nahodha wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta yamewazindua vijana wengi usingizini.

ZAMANI nikiwa mdogo, sikuwa nafahamu maana ya neno ‘Msanii ni kioo cha jamii’. Maneno haya kwangu yalikuwa ni sawa na misemo mingine ya wahenga. Zamani hizo, nikiwa vidudu nadhani, sikujua pia kuwa michezo mfano soka ni sanaa pia.
Sasa nimekuwa, macho yangu yamefunguka na kukubali kuyaona, sio maghorofa, nimegundua kumbe kila wakifanyacho wao (wasanii au watu maarufu), huko mitaani vijana wengi wanakaa chini mikononi wakiwa na kalamu na karatasi kujifunza.
Huwezi kunielewa ila usijali. Kabla hajawa maarufu, jina lake halijajulikana, kabla ulimwengu haujautambua uwezo wa miguu ya Mbwana Ali Samatta alikuwa kioo cha wachovu wenzake kule Mbagala.
Miaka kadhaa tangu atoke Simba, hadi kwa Wakongo kule TP Mazembe na sasa Ubelgiji kwa kina Eden Hazard, wala hakuwa kichochezi cha hasira za maisha kwa vijana wa rika lake.

Kalamu hii, inapoendelea kumwaga wino. Macho yako yanapoendelea kusoma makala haya, elewa kwamba, mafanikio ya nahodha huyu msaidizi wa KRC Genk na nahodha wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta yamewazindua vijana wengi usingizini.
Ndio, bisha ubishavyo lakini ukweli ndio huo. Vijana wengi sio Tanzania tu, bali dunia nzima, hasa wenye ndoto ya kucheza soka, wakimwaangalia Samatta, wanapata hamasa ya kuzidi kupambana. Akili na mioyo yao, inawaaminisha kuwa inawezekana.
Vijana wengi mitaani, shuleni, wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi nyingine za mataifa ya jirani, wamekuwa na ndoto ya siku moja kufikia mafanikio ya Samatta , ikiwamo kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa Ligi.
Samatta, mwenye umri wa miaka 26, anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, haijawahi kutokea.
Historia haifichi kwamba kumewahi kuwa na wanasoka wengine kutoka ukanda huu waliotisha kwenye michuano hiyo ya usiku wa Ulaya kama Wakenya Victor Wanyama aliyefika fainali msimu uliopita akiwa na Tottenham Hotspur, na kaka yake, McDonald Mariga, aliyebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Inter Milan chini ya kocha Jose Mourinho 2010.
Historia inawakumbuka vizuri tu na kuwapatia heshima pia. Ila ukweli utabaki kuwa, katika ukanda huu, hakujawahi kutokea kama Samatta. Namzungumzia mtu aliyefunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa usiku wa Ulaya, tena akiwa na kitambaa cha unahodha.
Pengine  umewahi kujiuliza kama mchezaji au mdau kuwa  ni mambo gani ya msingi  ambayo yanaweza kuifanya Tanzania kuwa na wachezaji katika daraja kama au zaidi ya Samatta wa sasa kama ilivyo kwa Mataifa ya Afrika Magharibi ambayo ukigusa Arsenal, Liverpool na klabu nyingine kubwa wana nyota kibao wanaokiwasha huko.

UMRI
Kwa mujibu wa CIES ambao wamekuwa wakitafuta na kufanyia uchunguzi takwimu za wanasoma mbalimbali, inadaiwa Kylian Mbappe wa PSG  ni miongoni  mwa  wachezaji  wenye thamani kubwa zaidi kipindi hiki kwa kuangalia pia umri wake wa miaka 20. Thamani yake ni zaidi ya Euro 281.5 milioni.
Samatta aliwahi kuposti katika mtandao wake wa Instagram kuonyesha vile alivyochelewa  kucheza soka la ushindani Ulaya, anatamani angekuwa KRC Genk  angali akiwa na umri mdogo.
Maana yake ni nini? Muda ambao anajiona kuwa katika kiwango bora zaidi ndivyo umri nao unavyomtupa mkono. Kimahesabu ana miaka minne hadi mitano akijitahidi kabla ya kuanza kuitwa mzee.
Unadhani kwa kiwango anachokionyesha sasa, ingekuwaje, kama angekuwa na umri wa miaka 19 au 20? Ni wazi angekuwa akigombewa na vigogo vya soka la Ulaya hivi sasa.
Umri sahihi wa kuanza kucheza soka Ulaya ni kati ya miaka 17 na 18 sio mbaya hata 19, ni ngumu kwa mchezaji mwenye miaka kuanzia 24 hadi 25 ambaye anacheza soka la ndani kutimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa Ulaya.

KANUNI
Kutofanya vizuri kwa Timu ya Taifa ya Tanzania, kunawafanya wachezaji wa Kitanzania wenye ndoto za kucheza soka Ulaya hasa katika ligi nne bora, England, Ufaransa, Ujerumani na Italia kuwa na safari ndefu ya kufikia ndoto zao.
Kwa mfano mchezaji mwenye kigezo cha kucheza Ligi Kuu England inatakiwa timu yake ya taifa iwepo katika viwango vya ubora wa soka duniani kuanzia nafasi ya 75 kwenda juu.
Ndio maana hata Victor Wanyama kwa kipindi kile baada ya kuondoka AFC Leopards ya kwao Kenya, alianza mizunguko kwa kuichezea, Helsingborg ya Sweden, Beerschot ya Ubelgiji na Celtic ya Scotland kabla ya kutua England ambako alijiunga na Southampton.
Kwa umri wa miaka 24 au 25 bado utapoteza miaka mingine katika klabu zenye viwango kama cha TP Mazembe na kwingineko ndio maana pointi ya umri inasimama kama msingi wa kucheza soka Ulaya.

UHUSIANO
Kupitia upenyo wa uhusiano wa ukaribu na klabu mbalimbali zilizoendelea barani Ulaya, inaweza kuwa moja ya njia ya kuwatengeneza kina Samatta wengine ambao wataanza kutanua wigo wakiwa na umri mdogo. Hapa hakuna mtazamo wa jicho la kibiashara zaidi pamoja na kuwa faida inaweza kupatikana.
Ukaribu unaweza kutoa nafasi ya japo mara moja kwa mwaka, kutoa vijana watatu hadi wanne kwenda kufanya majaribio ya kujiunga na akademi ya timu fulani, timu nyingi za Amerika ya Kusini zimekuwa zikitumia njia  hiyo.

BIASHARA
Klabu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara hazina maono ya kibiashara katika kupika vipaji na kuuza wachezaji. Kama klabu za hapa zingelenga mbali zingenufaika sana kwa kuuza wache-