Harmonize: Natamani kwenda Kigoma siku moja

Muktasari:

Harmonize amesema anatamani kwenda mkoani Kigoma, kwa kuwa hajawahi kufika.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Harmonize amesema anatamani kwenda mkoani Kigoma siku moja.

Harmonize ameyasema hayo leo Jumatano Januari 15, 2020 katika mkutano wa waandishi wa habari alipokuwa akitangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Twist.

Harmonize anayetesa na wimbo wa 'Uno' ameyasema hayo baada ya kuulizwa kama ziara yake ya kwenda kutangaza kinywaji hicho na wasanii wenzake itafika Kigoma.

"Sijawahi kufika Kigoma ila natamani nifike na nina imani nitafika siku moja," alisema Harmonize.

Katika ziara hiyo Harmonize atafanya maonyesho katika mikoa nane ambayo ni  Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Sumbawanga, Dodoma, Arusha, Mtwara na Kagera.

Wakati kuhusu ubalozi aliopewa wa kinywaji hicho cha twist, Harmonize alisema ameshukuru kwa kuaminiwa na kampuni hiyo ukizingatia kuwa wasanii waliopo ni wengi lakini amenekana yeye.

Hata hivyo amesema kabla yakukubali kuwa balozi amejidhihirisha utengenezaji wa bidhaa hiyo na upatikanaji wake ni wa uhakika ili asije akawaudhi mashabiki zake ambao wanaweza kutumia fursa hiyo kumtolea maneno machafu jambo ambalo hapendi.

Mwenyekiti wa kampuni ya Motisumn Group, Shubash Patel, amesema katika ubalozi huo msanii huyo kashiriki kuanzia  kubuni chupa, kuonja ladha na kueleza kuwa Harmonize sio tu msanii wa muziki ana vipaji vingi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kinywaji cha Sayona, Pawen Patel, amesema kupitia Harmonize wanaamimi watawafikia watu wengi ukizingatia ni msanii anayefanya vizuri ndani na nje ya nchi.