Hapo FKF kama mbaya mbaya tu Kenya

Thursday November 14 2019

Mwanaspoti-Hapo-FKF-kama-Tanzania-mbaya-mbaya-Kenya-ufisadi-uchaguzi-soka

 

By THOMAS MATIKO

BADO Rais wa Shirikisho la soka nchini FKF, Nick Mwendwa anazidi kukumbana na presha kutokana na ufichuzi wa ufisadi katika chombo hicho.
Baada ya kuanikwa jinsi alivyoharibu mamilioni ya pesa ya bajeti ya Sh244 milioni iliyotolewa na Wizara ya Michezo kwa FKF kugharimia maandalizi ya timu ya taifa ya Harambe Stars kwenye ushiriki wake wa dimba la AFCON 2019 kule Misri, sasa wanasiasa nao wamemkalia Mwendwa kikao.
Juzi kati Seneti ilifanya kikao kujadili uongozi wa Mwendwa katika shirikisho hilo, ambao waliushutumu kwa kukithiri na ufisadi.
Mada kubwa waliyojadili ni kuhusu uchaguzi mkuu wa FKF ulioratibiwa kufanyika Desemba 7 ambao sasa umezua mdahalo mkubwa.
Wagombea kadhaa Sam Nyamweya, Moses Akaranga, Alex Ole Magelo waliamua kutowasilisha skabadhi zao kwa bodi itakayosimamia uchaguzi huo wakidai tayari imeshapanga matokeo kwani iliteuliwa na Mwendwa.
Aidha walisema baadhi ya wanachama katika bodi hiyo ya uchaguzi ni wana ukaribu mkubwa na Mwendwa, hivyo hawana uhakika uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki.
Hata zaidi kumekuwa na mdahalo mkubwa kuhusu uamuzi wa FKF na bodi hiyo kuzifungia matawi 23 pamoja na wadau wengine kama vile Chama cha Marefa kutoshiriki uchaguzi huo.
Wakijadili kuhusu uchaguzi huo ambao huenda usifanyike kutokana na kesi mbili zilizowasilishwa zikitaka bodi hiyo ivunjwe.
“FKF ni chombo ambacho  Wakenya wengi wanahitaji kuwa na imani nacho lakini wamevunjwa moyo sababu ya uongozi wa sasa. Hawa ni mafisadi  hawastahili,” alisema Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula.
Mjadala huo uliibuliwa na Seneta wa Mombasa Faki aliyetaka taarifa kutoka kwa Wizara ya Michezo kuhusu jinsi uchaguzi huo wa FKF utakavyoendeshwa na ikiwa utakuwa wa huru na haki.
Faki aliiambia seneti ni klabu 18 pekee zilizoruhusiwa kushiriki uchaguzi huku zingine kutoka divisheni zote za soka nchini zikifungiwa
“Tungependa kufahamu ni kwa nini klabu 23 pamoja na tawi la FKF Mombasa zimezuiliwa kushiriki kwenye uchaguzi.”
Akiunga hoja hiyo Seneta wa Siaya James Orengo alisema uongozi wa sasa wa FKF upo katika mikono ya matapeli wasiona nia ya kuboresha soka.
“FKF ya sasa ni aibu tu. Soka haiwezi kuendeshwa na serikali kwa sababu sheria za FIFA haziruhusu lakini pamoja na hayo hatuwezi kuuachia uongozi wa soka makateli. Wanaumiza hali ya soka nchini,” Orengo akatia lake.
Sasa kamati hiyo imeitisha kikao na Mwendwa aweze kuelezea kwa kinaga ubaga ni kwa nini uongozi wake umekuwa wa hati hati na nia yake ni nini hasa.

Advertisement