VIDEO: Diamond apokewa na mabango akiwasili Kigoma

Sunday December 29 2019

Mwanaspoti-Diamond-Tanzania-apokewa-treni-Kigoma-mabango-akiwasili-Kigoma

 

By Nasra Abdallah

Kigoma.Mwanamuziki Diamond Platnumz amepokewa na mabango wakati akiwasili stesheni ya Nguruka Mkoani Kigoma katika kuadhimisha miaka yake kumi katika muziki.

Umati wa watu umejitokeza katika stesheni ya Nguruka Mkoani Kigoma wakiwa na mabango yaliyobeba jumbe mbalimbali kwa mwanamuziki huyo.

Moja ya mabango hayo lilikuwa limeandikwa “Karibu Diamond kwenu Kigoma tuijenge Kigoma, Sisi Nguruka tulishaanza ujenzi wa madarasa saba na vyoo 12. Tunaomba tuunge mkono, watoto 494 hawana pakusoma.”

Diamond aliyeanza safari ya kuelekea Kigoma jana Desemba 28, 2019 akiwa na mashabiki wake katika treni lengo lake kubwa ni kujumuika na watu wa mkoa huo kusheherekea miaka kumi tangu kuanza muziki.

Nguruka ikiwa ndio stesheni ya kwanza unapoingia Mkoa wa Kigoma, Diamond alikutana na umati wa watu ukimsubiri.

Advertisement

Tofauti na stesheni nyingine alizopita katika mikoa ya Morogoro, Singida na Tabora, Kigoma walionekana kijiiandaa vilivyo ikiwemo kumtengenezea jukwaa na kujikusanya mithili ya watu wanaosubiri mkutano wa hadhara.

Baada ya kuwasili eneo hilo Diamond alipanda jukwaani na kuanza kuwaimbisha wakazi hao wimbo wa Baba lao ambao umeonekaba kuiteka safari nzima kila alipopita kwa kuwambia mashabiki zake anapowakuta stesheni.

Hata hivyo ilifika mahali mzuka ukampanda kweli kama moja ya kibwagizo kilichopo katika wimbo huo kinachosema 'mzuka ukipanda hata nguo nitavua, nivue muone'walipoitikia mashabiki akavua fulana yake aliyokuwa ameivaa ambapo watu wake waliichukia na baadaye kumrudishia.

Pia Diamond alitumia nafasi hivyo kuwaita jukwaa hilo lililokuwa limepambwa kwa vitambaa vya rangi nyeupe na nyekundu, wasanii wengine wa lebo ya wasafi akiwemo Queen Darleen, Lavalava, Rayvanny na Young Killer ambaye kaacha maswali huenda ikiwa ni wasanii wanaotarajia kuwasajili.

Wasanii hao wote walitumbuiza kwa muda wa dakika 30 kisha kuendelea na safari huku Diamond akiwataka wasikose show ya Desemba 31, 2019 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Advertisement