Chambua ajitosa kumtetea Samatta

Muktasari:

Nyota wa zamani wa timu ya Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua amemtetea nahodha wa timu ya Taifa Mbwana Samatta kuwa anastahili pongezi siyo kunezwa.

Dodoma.Nyota wa zamani wa timu ya Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua amesikitishwa na matamshi ya baadhi ya mashabiki wanaombeza nahodha Stars, Mbwana Samatta akisema kufanya hivyo ni kutomtendea haki.

Akizungumza Jijini Dodoma leo Novemba 24, 2019 Chambua amesema kauli za baadhi ya mashabiki siyo kwamba zinalenga kumpunguzia juhudi Samatta, lakini zinamchonganisha na wachezaji wenzake.

Nyota huyo aliyeichezea Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo, alisema kauli za kumbeza Samatta kwamba hajitumi anapokuwa na timu ya taifa, hazina ukweli na wanaotoa kauli hizo hawaangalii uwepo wake uwanjani kama ni moja ya kuwapunguza matumaini washindani wao.

“Mimi nimecheza mpira na nimeacha kwa heshima yangu, lakini nataka watu wajue kuwa mpira kuna siku unaweza kukataa, sasa wanachukulia siku moja na kumhukumu, hebu waangalie namna anavyopambana katika mechi zingine hata kulazimisha mabao ya nguvu kupitia kwake, inauma, na inaumiza kweli,” alisema Chambua.

Hata hivyo amesifu kauli aliyoitoa Samatta kuwa alipokea changamoto zinazoelekezwa kwake na anazichukulia kama sehemu ya kurekebisha makosa akisema ni kauli ya mtu aliyekomaa hivyo kumtaka asipate hasira kwani bado nafasi ya timu hiyo ni nzuri.

Akizungumzia kikosi cha Stars kwa ujumla wake, amesema ni kizuri na hakihitaji marekebisho badala yake juhudi za wachezaji na kutobweteka wawapo uwanjani.

Alisema vijana hao kwa kocha Ndayiragije wanaweza kufika mbali ikiwa wataamua kucheza kwa kutaka kung’ang’ania namba na kuwa wajisikie maumivu wasipopata nafasi.