Chama amlilia Aussems Simba

Monday December 2 2019

Mwanaspoti-Chama-amlilia-Aussems-Simba SC-Tanzania-soka-Ligi-Kuu-Bara

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Kiungo wa Simba, Clatous Chama amemtakia kila la heri aliyekuwa kocha wake Patrick Aussems baada ya kufutwa kazi katika timu hiyo aliyoitumikia kwa mwaka mmoja na nusu.
Chama  ambaye ni Mzambia, alisema Aussems ni kati ya makocha bora ambao amepata nafasi ya kufanya kazi nao hivyo itamchukua muda  kusahau uwapo wake.
“Nakumbuka vile tulivyoweza kuvisumbua vigogo vya soka la Afrika, tulivyokuwa tukipoteza michezo  ya ugenini, tulijiona tunaanza upya tukiwa  nyumbani. Namtakia kila la heri huko aendako,” alisema nyota huyo wa Simba.
Simba ikiwa chini ya Aussems ilitinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambapo ilitolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-1 na TP Mazembe ya DR Congo.
Ilianza kwa kuitoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1 na katika hatua ya kwanza wakaitupa nje Nkana FC ya Zambia kwa kuichapa jumla ya mabao 3-2 kisha wakatinga hatua ya makundi ambapo waliangukia katika kundi D lililokuwa na timu za Al Ahly, AS Vita Club na JS Saoura.
Katika hatua hiyo ya makundi walimaliza wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Al Ahly wakikusanya pointi tisa baada ya kupata ushindi katika mechi tatu na kupoteza tatu kabla ya kukwaa kigingi mbele ya Mazembe katika robo fainali.

Advertisement