Ambokile: Naleta ya Mazembe Kilimanjaro Stars

Monday December 2 2019

Mwanaspoti-Ambokile-Naleta-Mazembe-Kilimanjaro-Stars-Tanzania-Chalenji-Cecafa

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam.  Mshambuliaji wa TP Mazembe, Eliud Ambokile amesema kuitwa timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ni ishara nzuri kwake kutokana na shauku aliyonayo ya kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Ambokile ambaye anakumbana na changamoto ya namba katika kikosi cha kwanza cha TP Mazembe, alisema ameipokea kwa mikono miwili nafasi  ya kuitwa Kilimanjaro Stars.
“Nipo katika kipindi kigumu lakini nimekichukulia kwa mtazamo chanya kama sehemu ya kujituma zaidi,  kuna mechi ambazo nimekuwa nikipata nafasi ya kucheza, nyingine nimekuwa  nikiishia  kakaa benchi.
“Hivyo sikuwa na nafasi ya kutosha kuonyesha uwezo wangu, pamoja na hayo ninajiona kuwa na furaha Mazembe kwa sababu tupo kwenye kutengenezwa, isitoshe huu ndio kwanza msimu wetu wa kwanza. Nimefurahi kuitwa Kili,” alisema Ambokile akiahidi kuleta aliyojifunza kule TP Mazembe.
Pamoja na Ambokile, washambuliaji walioitwa katika kikosi cha Kilimanjaro Stars ni Paul Nonga (Lipuli FC), Miraji Athuman ‘Sheva’ (Simba SC), Shaaban Iddi Chilunda (Azam FC).
Wengine ni Ditram Nchimbi (Polisi Tanzania), Kelvin John (Football House), Eliuter Mpepo (Buildcon/Zambia) na Lucas Kikoti (Namungo FC).
Ambokile alijiunga na Mazembe akitokea Mbeya City.

Advertisement