Shikhalo atoboa siri ya kukaa benchi Yanga amtaja Mechata

Sunday March 22 2020

Mwanaspoti, kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo, Tanzania, Corona, akitokea Bandari ya Kenya

 

By KHATIMU NAHEKA

KIPA wa Yanga, Farouk Shikhalo ameweka wazi bado hajapewa nafasi ya kuonyesha ubora wake uliomleta Tanzania.
“Tangu nifike Tanzania maisha yangu kwa kiasi fulani yamekuwa na changamoto mbalimbali na kitu cha kwanza ni kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, sijapata nafasi ya kuonyesha kile ambacho binafsi nakijua ninacho katika ubora wangu,” anasema kipa huyo Mkenya aliyesajiliwa Yanga akitokea Bandari ya Kenya.
Shikhalo ni mmoja kati ya makipa wawili wa Yanga waliosajiliwa msimu huu kuja kuimarisha eneo la kulinda lango la timu hiyo akibeba matumaini makubwa.
“Unajua nafasi ya kipa ni tofauti sana unatakiwa kipa upate nafasi mara kwa mara ndio ubora wako unaongezeka zaidi na kwa haraka na hiyo ndio duniani kote ipo hivyo lakini bado siwezi kukata tamaa muhimu ni kuongeza juhudi katika kupambana zaidi ili nilinde ubora wangu.
“Ni kama sijaingia uwanjani kuisaidia hii timu kitu naweza kuangalia labda naweza kusema tangu nimefika hapa ni mechi moja pekee ndio nimeweza kufanya kitu nikasema ndio, huyu ndio Shikhalo na ni ile mechi dhidi ya Simba lakini kijumla bado sijaweza kujipambanua kama ninavyojijua kikubwa nasubiri nafasi.”

Kipi kinamnyima nafasi?
“Hapa kuna makipa watatu ingawa tumekuwa tukipishana sana mimi na mwenzangu Mnata (Metacha) lakini inawezekana labda kwa kuwa nashindana na mwenzangu ambaye hapa ni nyumbani kuna mambo mengi yanaweza kutokea katika yupi atangulie.
“Mimi niko tofauti sitaweza kupotea kwa kukaa benchi, ninapokaa benchi huwa nachukulia ni sehemu ya kujifunza kitu, mara nyingi huwa ninapokaa benchi huwa naongeza nguvu ya kupambana kuanzia kwenye timu mpaka katika mazoezi yangu binafsi, siku nikipata nafasi nakuwa Shikhalo yuleyule.

Anamwonaje Mnata?
“Metacha ni mmoja kati ya makipa wazuri hapa Tanzania ambao nimekutana nao,ana uwezo lakini pia ni kipa mzuri ambaye anaweza kukupa ushindani ukajituma kupitia juhudi zake,ukiwa katika timu ukakutana na kipa mzuri anaweza kukusaidia kufikia malengo yako ingawa bado naamini katika ubora wangu, mimi sio mtu wa kuogopa ushindani.”

Ilikuwaje AKAJA Yanga
“Haikuwa rahisi kufanya maamuzi ya kuja hapa Tanzania hasa Yanga ingawa nakiri Yanga ndio klabu ambayo ilinifuatilia kwa muda mrefu kuliko timu zote tatu kutoka nje ya Kenya.
“Unajua kabla ya kuja hapa Yanga nilikuwa katika kikosi cha Kenya kilichocheza Afcon kule Misri lakini pia nilitoka kuwa kipa bora wa Kenya katika ligi mara mbili, kwa hiyo wakati namaliza Afcon timu mbili mbali na Yanga zilikuwa zinanihitaji kama Zesco ya Zambia, Botswana hapa Tanzania na hata Bandari hawakutaka nitoke.
“Mimi nilisaini nikiwa Misri nakumbuka aliponifuata kiongozi Kamugisha (Frank) alitaka kabla hajaondoka lazima nisaini mkataba. “Pale kambini kulikuwa na ulinzi sana lakini ukiacha hilo kocha Migne alijua Yanga wananihitaji na hakutaka nisaini kwao kwa kuwa alitaka nibaki Bandari ili nicheze timu yake kuwania fainali za Chan na nakumbuka tulitakiwa kukutana  na Tanzania.”

kipa VS beki
“Kuna wakati safu ya ulinzi inaweza kumbeba kipa lakini mimi kwa upande wangu siamini sana mabeki kumbeba kipa ninachoamini kipa ndio anastahili kuwabeba mabeki, nasema hivi kwa sababu ukiwa kipa mzuri mabeki watafanya makosa na wewe utawazibia, lakini ikitokea mabeki wakafanya makosa na kipa akawa mbovu lazima timu itapoteza, mnaweza kuwa na timu mbovu lakini kipa akaibeba timu na imetokea sana kwangu.

Makipa watatu timu za taifa
Yanga ina makipa watatu ambao ni Ramadhan Kabwili wa timu za vijana, Mnata na Shikhalo mwenyewe na hapa anaelezea ugumu unapokuja; “Hii ndio shida kubwa kila kipa hasa sisi wawili (Mnata) kila mmoja anatakiwa kutafuta nafasi ya kucheza timu ya taifa lake,bahati nzuri mwenzangu anacheza katika ardhi ya nyumbani kuna mengi yanaweza kutokea.”

Ushindani wa ligi VIPI?
“Ligi ya Tanzania ushindani wake ni mzuri, ligi ambayo inaweza kukuuza,kitu ambacho kinaipa ubora ligi ya hapa ukilinganisha na kule kwetu ni kwamba hapa ligi inaonyeshwa ‘live’ hii ni nafasi nzuri inatoa fursa kwa makocha na mawakala kufuatilia vipaji lakini hata ushindani upo pia.

Changamoto ya soka la bongo ni ipi?
“Kikubwa hapa wanatakiwa kurekebisha mambo ya waamuzi wanaharibu ubora wa ligi ya hapa,kuna wakati unaona matukio kisha ukajiuliza huyu aliyefanya maamuzi haya ni mtu aliyefundishwa na akafuzu kweli? Lingine hapa watu wanaongea sana, ukicheza hapa natakiwa kuweka vizuri masikio yako kwa kutofuatilia sana nini watu wanaongea
“Kuhusu viwanja hapa kuna viwanja vingi lakini vingi sio bora kule Kenya kuna viwanja vichache lakini ni bora kuna kitu kinanishangaza hapa ukiangalia viwanja vya mjini ukiondoa kile cha Taifa ni vizuri kuliko vile vya mikoani lakini kule kwetu ni kinyume chake kule mikoani ndio kuna viwanja vizuri kuliko vya mjini.”

UBINGWA Yanga
“Kusema ukweli ni vigumu kwa msimu huu Yanga kupata nafasi ya kuchukua kombe la ligi kuna makosa mengi tulifanya katika hesabu zetu huko nyuma lakini mimi kama Shikhalo ukiniuliza kipi natamani sasa ni kuisaidsia timu yangu angalau kupata kombe la FA kama tukiweka juhudi kubwa hili haliwezi kutushinda, angalau hili linaweza kuwapa faraja mashabiki wetu, pia itatusaidia kupata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa ya Afrika msimu ujao.”

Jamaa kwa ugali acha kabisa
Akizungumzia ratiba ya chakula chake Shikhalo anasema: “Chakula ninachopenda hasa ni ugali kule ninakotokea ugali ndio chakula kikubwa tunakula usiku, napenda sana kula ugali na kuku nilipofika hapa nilishangaa kusikia ugali unaliwa mchana naweza kula chochote kama ni wali au tambi, pia ninapokuwa nimefanya sana mazoezi binafsi napenda sana kupata matunda mengi.

usajili Yanga
“Maoni yangu naona eneo kubwa ambalo makocha wanatakiwa kuliangalia kwa jicho la umakini ni safu ya ushambuliaji, nimeangalia msimu huu tumefunga mabao machache sana hii inaonyesha hatukuwa na ubora katika kutumia nafasi.
“Tunahitaji washambuliaji wenye kasi kubwa ya kufunga Yanga inatakiwa kuwa na washambuliaji ambao hawawezi kumaliza mechi mbili hajafunga,timu inatakiwa kuwa na washambuliaji ambao kila ukisikia tumepata mabao mawili unauliza flani amefunga?Tukipata watu sahihi tutakuwa sawa sana msimu ujao.

Makipa anaowakubali
“Kama nilivyosema Mnata sio kipa mbovu ni kipa mzuri kwahiyo kwa nafasi anayopata sasa naona anaweza kuwa kipa ambaye ananivutia, pia namkubali sana Manula ni kipa ambaye namjua anajuhudi ingawa hana bahati ya kupendwa sana na mashabiki wa hapa.”

Advertisement