VIDEO: Yanga ya Eymael ni mwendo wa saresare maua Ligi Kuu Tanzania Bara

Muktasari:

Yanga inarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuliwahi pambano lao la Kombe la FA dhidi ya Gwambina kabla ya kuikaribisha Alliance na Mbao kutoka Mwanza katika mechi zao zijazo kisha kuvaana na watani zao katika Kariakoo Derby itakayopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Taifa.

MNAHESABU lakini? Sare ya nne mfululizo iliyopata Yanga jana Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga walipovaana na Coastal Union, imeifanya timu hiyo kuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha inashinda mechi saba mfululizo, kama inataka kuzifikia pointi walizonazo watani wao.
Sio kushinda mechi hizo saba ili kuvuna alama 21, lakini pia italazimika kuiombea Simba ipoteze mechi zenye idadi kama hiyo, kati ya 14 walizosaliwa nazo, jambo ambalo linahitaji miujiza kuweza kutokea kutokana na kasi waliyonayo Wekundu wa Msimbazi hao wanaoongoza msimamo kwa sasa.
Ikiwa imetoka kuambulia sare ya 1-1 na Polisi Tanzania mjini Moshi, Yanga jana ilishindwa kufanya maajabu mbele ya Wagosi katika pambano kali lililomalizika kwa suluhu ambayo imezidi kuwapa wakati mgumu mashabiki wa Yanga ya kuona timu yao inarejesha taji la Ligi Kuu msimu huu.
Matokeo ya jana yameifanya Yanga kukusanya pointi 41 ikibaki nafasi ya nne, nyuma ya Namungo yenye alama 43 na Azam wanaokamata nafasi ya pili na alama zao 45, huku Simba ikiwa kileleni wakikusanya pointi 62. Hata hivyo Yanga ina michezo miwili mkononi kuweza kuwafikia wapinzani wao ambao wanalisaka taji la tatu mfululizo katika ligi hiyo ya Bara iliyoasisiwa mwaka 1965.
Kocha Luc Eymael aliyewaanzisha tena kwa pamoja, Tariq Seif na Ditram Nchimbi, amejikuta akivuna pointi nne tu kati ya 12, huku akipoteza nane ambazo pengine kama wangezipata zingewaweka kwenye nafasi ya pili na kuwapumulia watani wao.
Mbali na Wagosi na Polisi, Yanga pia ililazimishwa sare dhidi ya Tanzania Prisons waliotoka nao suluhu na kuambulia sare ya 1-1 walipovaana na Mbeya City.
Katika mchezo huo wa jana kipa wa Yanga, Metacha Mnata, alifanya kazi ya ziada kuokoa michomo hatari ya wapinzani wao kupitia  Ayoub Semtawa dakika ya 25 na 85 na kombora la Ayoub Lyanga dakika ya 69.
Fundi wa mpira, Mghana Bernard Morrison kama kawaida yake aliendelea kuwapa burudani mashabiki wa namna alivyokuwa akiwatesa mabeki wa Coastal, akisaidiana nyota wengine wa Yanga ambao walikatwa stimu na kipa wa Coastal Union, Soud Abdallah.
Makocha Juma Mgunda wa Coastal na Eymael wote walifanya mabadiliko kipindi cha pili, lakini hayakuwa na faida yoyote licha ya kuwepo kwa kosa kosa nyingi, huku wenyeji wakipoteza nafasi muhimu dakika za jioni walipopata frii-kiki ambapo Lyanga alipaisha mpira.
Kocha Eymael aliwatoa Mapinduzi Balama, Tariq na Haruna Niyonzima na kuwaingiza Mrisho Ngassa, Ally Mtoni ‘Sonso’ na Mzambia Erick Kabamba.
Coastal nao walimtoa Mudathir Said na kumuingiza Haji Ugando ambaye aliwasumbua mabeki wa Yanga waliokuwa wakiongozwa na Mghana Lamine Moro na Said Juma ‘Makapu’.
Yanga inarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuliwahi pambano lao la Kombe la FA dhidi ya Gwambina kabla ya kuikaribisha Alliance na Mbao kutoka Mwanza katika mechi zao zijazo kisha kuvaana na watani zao katika Kariakoo Derby itakayopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Taifa.

PRISONS YAZINDUKA
Katika mechi nyingine za ligi hiyo jana, maafande wa Tanzania Prisons wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma waliitambia Lipuli FC kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Salum Kimenya dakika ya 10 na Ismail Aziz dakika ya 90, huku Alliance wakibanwa nyumbani na Singida United kwa kutoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza. Alliance walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 12 lililofungwa na Sameer Vincent kabla ya Mghana Steve Opoku kusawazisha dakika ya 53.
Mechi zijazo za Yanga
-Feb 26 v Gwambina
-Feb 29 v Alliance
-Mar 03 v Mbao
-Mar 08 v Simba