Huku Yanga ni Morrison, kule Simba Luis hapatoshi

Muktasari:

Yanga ilimsajili Morrison aliyewahi kukipiga Orlando Pirates ya Afrika Kusini na AS Vita, DC Motema Pembe za DR Congo kama mchezai huru, huku Simba ilimsajili Luis kutoka UD Songo ya Msumbiji akikokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns.

YANGA ilianza kutamba na Bernard Morrison na vile vimbangwa vyake vya kutembea juu ya mpira. Simba wakanuna, lakini baada ya Luis Jose Miquissone kukipiga katika kiwango cha hali ya juu juzi Jumamosi dhidi ya Biashara United, Msimbazi sasa ni kicheko.
Wameipata fimbo ya kuwanyamazisha watani wao ambao waliwanyima raha kwa siku kadhaa kwa kuliimba jina la Morrison na shibobo yake.
 Hata hivyo kumbe nyota hao waliosajiliwa na timu hizo katika dirisha dogo la usajili, wanatofautiana sana licha ya wote kuwa na vipaji.
Yanga ilimsajili Morrison aliyewahi kukipiga Orlando Pirates ya Afrika Kusini na AS Vita, DC Motema Pembe za DR Congo kama mchezai huru, huku Simba ilimsajili Luis kutoka UD Songo ya Msumbiji akikokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns.
Hata hivyo, naye Luis ambaye anang’ara kwa kuchezesha timu, pasi za mwisho na kufunga.

MORRISON
Thamani yake ni Euro 175 na ilikuwa juu zaidi mwaka 2016 alipokuwa na Orlando Pirates ambayo ni Euro 250.
Ndani ya Yanga amefunga mabao mawili, pasi mbili za mabao kwenye mechi sita alizocheza ya FA dhidi ya Tanzania Prisons wakashinda 2-0, alifunga bao na akatoa pasi ya bao, Singida United wakashinda 3-1 alitoa pasi ya goli, Mtibwa Sugar walishinda 1-0, Lipuli FC wakashinda 2-1 alifunga bao, Mbeya City sare 1-1 akafunga bao, Tanzania Prisons wakasuluhu.
Alizaliwa Januari 25, 1993, Mankessim, Ghana, sasa miaka 27, Ghana. Anacheza nafasi ya ushambuliaji wa kati na winga wa kushoto.
Klabu alizocheza, Heart of Lion, Ashanti Cold za Ghana, AS Vita Club, DC Motema Pembe za DR Congo, Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Ajenti wake ni KC Sports Marketing Management.

LUIS NAYE NOMA
Thamani yake ni Euro 150k hajawahi kuzidi.
Ndani ya Simba, amecheza mechi tano amefunga bao moja na kutoa pasi ya bao moja.
Amezaliwa Mei 25, 1995, Msumbiji, anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na winga wa kulia, anatumia zaidi mguu wa kushoto na kidogo kulia.
Amecheza mechi tano dhidi ya JKT Tanzania wakafungwa 1-0, Mtibwa Sugar wakashinda 3-0, Lipuli FC walishinda 1-0 aliingia, Kagera wakashinda 1-0 kwa penalti, Biashara United wameshinda 3-1, ametoa pasi ya bao na kufunga.
Klabu alizopita UD Song ya Msumbiji, Mamelodi Sandowns, Chippa United na Royal Eangles za Afrika Kusini. Ajenti wake Wimbi Foot.

 WADAU SASA
Nyota wa zamani wa kimataifa ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka,  Ally Mayay amesema, aina ya mpira wa Luis na Morrison unafanana.
“Wanapokuwa na mpira wanakuwa wazuri zaidi na mchango wao unaonekana na uwanjani wanacheza wakiwa huru, lakini timu inapokuwa haina mpira uwezo wao wa kukaba ni mdogo,” alisema Mayay.
“Ubora wao wa ubunifu na kasi uko juu. Ni watu wa kujitoa na kuthubutu kwa sababu ni wabunifu, ila hapa kwa Morrison kuna utofauti kidogo na Luis. Morrison anakuwa mtu wa kuriski zaidi hata kama sehemu hiyo hakutakiwa kufanya hivyo. Yaani anaweza kulazimisha shambulizi apite mwenyewe wakati angetoa pasi kwa mwenzake ingekuwa na faida kubwa zaidi, mwenzake hajafanya hivyo.”
Alisema, ubunifu wao huo, ndio umekuwa ukiwasababishia mabeki wa timu pinzani kuwachezea madhambi zaidi wanapokuwa na mpira.
Naye Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’ alisema, aina ya uchezaji wao unafanana.
“Wote ni mafundi, wanacheza mpira wa kisasa unaotakiwa duniani. Ni msaada kwenye timu, juhudi zao binafsi zinawabeba na hii ni kwa sababu wanajua kuchezea mpira. Suala la kukaba timu inapokuwa haina mpira hapo kuna mambo mawili, inategemea na makocha wao wamewapa majukumu gani,” alisema Bares.