Yanga yamsaka mshambuliaji wa DC Motema Pembe

Muktasari:

Bonganga anamaliza mkataba wake na Motema Pembe mwisho wa msimu huu na amegoma kuongeza kwa vile Yanga wameshamtupia chambo.

YANGA imeanza mchakato wa kuwashawishi mastraika wawili kutoka DR Congo kwa ajili ya  msimu ujao wa Ligi Kuu Bara. Tafsiri yake rahisi ni siku za Muivory Coast, Yikpe Gnamein zinahesabika Yanga.
Kocha Luc Eymael amewaambia Yanga anajua watupiaji wa maana ambao wanaweza kufuta ukame wa mabao Jangwani.
Straika wa kwanza ambaye Mwanaspoti limepewa jina lake na kigogo wa Yanga ni Vinny Bongonga wa DC Motema Pembe ya DR Congo ambaye anashika nafasi ya pili katika msimamo wa ufungaji nchini humo akiwa ametupia mara 10.
Katika msimamo wa mabao Bonganga ametanguliwa na Jackson Muleka wa TP Mazembe mwenye mabao 12 ambaye ni ngumu kutua Yanga kwa vile kabla bingwa wa Tanzania hajapatikana msimu huu jamaa atakuwa anakipiga Ulaya.
Habari njema kwa Yanga ni,   Bonganga anamaliza mkataba wake na Motema Pembe mwisho wa msimu huu na amegoma kuongeza kwa vile Yanga wameshamtupia chambo.
Mbali na Bonganga pia Eymael amemuweka kwenye rada zake, Lelo Patrick anayeichezea AC Rangers ya DR Congo ambaye msimu huu tayari ameshaifungia timu hiyo mabao tisa.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni, mmoja kati ya washambuliaji hao huenda akachukua nafasi ya Yipke Garmien ambaye hakuna kigogo yoyote anayemkubali baada ya kugundua ni mchezaji wa kawaida sana.
Habari zinasema uwezekano wa Yikpe kubaki Yanga haupo na kinachosubiriwa ni msimu umalizike miezi mitatu ajayo asepe zake Eymael asuke upya safu yake.