Washambuliaji Bongo tripu shamba-tripu gereji

Sunday February 16 2020

Mwanaspoti, Washambuliaji Bongo, Tanzania, Mwanasport, Simba, Yanga, Azam,

 

By CHARITY JAMES

WAKISIKIA wanaweza kurusha ngumi. Lakini ndio ukweli takwimu haziongopi. Mastraika wazawa kwenye Ligi Kuu Bara wamekuwa kama gari la mkaa. Tripu moja shamba tripu moja gereji, hiyo ni baada ya mastaa hao kushindwa kuendeleza rekodi zao kwenye upachikaji mabao kwa kila msimu.
Takwimu za maktaba ya Mwanaspoti kwenye misimu mitatu mfululizo zinaonyesha hawana rekodi nzuri kwenye nafasi hiyo kutokana na kila msimu kuibuka na nyota wengine tofauti na msimu ya nyuma.
Ndani ya misimu hiyo mitatu vinara wa upachikaji mabao ni nyota wa kigeni huku wao wakijaribu kuingia kwenye kumi bora ndani ya misimu hiyo mitatu mfululizo msimu wa mwaka 2017/18, Emmanuel Okwi ndiye aliyekuwa kinara kwa kuingia nyavuni mara 20.
Msimu huo mzawa John Bocco, Marcel Boniventure walishika nafasi ya pili kwenye upachikaji wa mabao baada ya kuingia kambani mara 14 nafasi ya tatu ilikamatwa na Obrey Chirwa ambaye alifunga mabao 12 nafasi ya nne ni mzawa Mohammed Rashid ambaye alitupia kumi.
Nafasi ya tano ilikuwa ni ya wazawa pia ambao waligongana watatu wote wakiwa na mabao tisa ambao ni Habib Kyombo (Mbao), Eliud Ambokile (Mbeya City) na Shaaban Idd Chilunda (Azam), wakati Paul Nonga (Mwadui), Adam Salamba (Lipuli), Khamis Mcha ‘Vialli’ (Ruvu Shooting) wao walifunga manane na Ibrahim Ajib (Yanga), Shiza Kichuya (Simba) na Asante Kwasi (Simba) walifunga mabao saba.
Msimu uliofuata nyota wengi hawakuchezea timu zao kutokana na kufanya vizuri na kujikuta wanahamia timu nyingine na kupotezwa kabisa kwenye rekodi ya upachikaji wa mabao isipokuwa wale wa kigeni ambao walibaki kwenye timu zao.
Emmanuel Okwi alikutana na mkali wa kufumania nyavu na kumtoa kwenye nafasi yake ambaye ni Meddie Kagere na msimu wake wa kwanza kutua Simba aliingia kambani mara 23 na kutwaa kiatu cha dhahabu na nafasi ya pili ilishikiliwa na Salum Aiyee akiwa (Mwadui FC) mabao 18, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na mchezaji wa kigeni, Heritier Makambo akiwa Yanga. Alitupia mabao 17.
Nafasi ya nne ilichukuliwa na mzawa John Bocco ambaye aliingia kambani mara 16 na Emmanuel Okwi akiingia kambani mara 15, Dickson Ambundo aliingia mara 12, Donald Ngoma mara 11 wakati Said Dilunga, Eliud Ambokile, Vitalis Mayanga, Jaffar Kibaya, Habib Kiyombo Idd Seleman wote wakitupia mara kumi.
Msimu huu nyota wote waliofanya vizuri mwaka jana na kuhama kwenye timu zao wamejikuta wanapotea kabisa kwenye rekodi za upachikaji wa mabao na wageni wameendelea kuwa viwembe kwa mabeki.
Ni mzunguko wa pili sasa unaendelea Kagere anashikilia rekodi ya upachikaji wa mabao na wazawa aliokuwa nao kwenye rekodi nzuri ya upachikaji wa mabao wamepotea na kuibuka wapya ambao ni pamoja na Reliants Lusajo (Namungo) ambaye ameingia kambani mara tisa akifuatiwa na Paul Nonga (Lipuli) Daruwesh Saliboko (Lipuli) Yusuf Mhilu (Kagera) wote wana mabao manane.
David Molinga (Yanga) ni kama amebadili utawala wa Okwi ambaye ametimkia Misri baada ya kushika nafasi ya pili kwa nyota wa kigeni akiwa na mabao saba akifukuzana na Obrey Chirwa (Azam). Wazawa wengine walioingia mara sita kambani ni Athuman Miraji (Simba), Wazir Junior (Mbao), Ayoub Lyanga (Coastal Union), Adam Adam (JKT Tanzania), Peter Mapunda (Mbeya City) na Hassan Dilunga (Simba).

Advertisement