Kisa corona: Suarez alisha familia 500 huko kwao Uruguay

Muktasari:

Maelfu ya watoto huko Uruguay wanaotoka kwenye familia masikini amekuwa wakitegemea chakula cha bure kinachotolewa shuleni, hivyo Suarez amelifikiria zaidi kundi hilo linaishi vipi kwa wakati huu wakati shule hizo zikiwa zimefungwa.

BARCELONA, HISPANIA. Kutoa ni moyo. Wanasema ukiwa nacho gawana na wengine. Straika supastaa, Luis Suarez anasaidia kuzilisha familia 500 za huko kwao Uruguay katika kipindi hiki cha janga la virusi vya Corona.
Fowadi huyo wa Barcelona amekuwa akiwasiliana na mamlaka za serikali huko kwao Uruguay kujaribu kutoa msaada wa kuwalisha watoto kwenye tatizo la njaa baada ya serikali kuamua kufunga shule zote kama tahadhari ya kuzuia maambukizi hayo ya Corona.
Maelfu ya watoto huko Uruguay wanaotoka kwenye familia masikini amekuwa wakitegemea chakula cha bure kinachotolewa shuleni, hivyo Suarez amelifikiria zaidi kundi hilo linaishi vipi kwa wakati huu wakati shule hizo zikiwa zimefungwa.
Kutokana na hilo ameamua kugawa msaada wa vyakula hasa kwa wananchi wanaoishi Casavalle, kaskazini mwa jiji la Montevideo.
Vikapu anavyotoa Suarez vinakuwa na vyakula vyote muhimu pamoja vifaa vya usafi kama sabuni.
Suarez alisema: “Walau naweza kufanya kitu kidogo kwa watu wenye uhitaji.”
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool, mwenye umri wa miaka 33 amegoma kuondoka Hispania licha a nchi hiyo kuwa miongoni mwa zilizothirika zaidi na maambukizi ya virusi hivyo vya Corona.
Staa huyo kwa sasa anapona majeraha yake ya upasuaji wa goti aliofanyiwa Januari na ameamua kubaki Hispania huku akifanya kila analoweza kusaidia nchini kwao Uruguay.
Amesema amegoma kurudi kwao Amerika Kusini kwa sababu ya kuwapo kwa changamoto nyingi za huduma za kiafya za jamii na hivyo kuamua kubaki zake Ulaya.
“Hakijawahi kuja kitu cha kurudi nyumbani kwetu kwenye akili yangu kwa sababu nadhani njia nzuri zaidi ya kuwasaidia Wauruguay sio mimi kurudi nyumbani,” alisema.
“Kama nahitaji kusaidia, basi nitafanya hivyo nikiwa hapa. Nitafanya hivyo kwa kujivunia kabisa kama itahitajika kufanya hivyo.
“Nawafikiria watoto wangu, nafikiria kuhusu tahadhari iliyotolewa ya kutakiwa kujifungia ndani ya kuepuka mkusanyiko wa watu.
“Maamrisho ya serikali na wataalamu mbalimbali yanasema tubaki nyumbani na hicho ndicho kitu kinachopaswa kufanywa na kila mtu.”
Mchezaji mwenzake Suarez kwenye klabu ya Barcelona, Lionel Messi ametoa msaada mkubwa wa pesa kiasi cha Euro 1 milioni kusaidia taasisi zinazojishughulisha kwa karibu kwenye janga la virusi vya Corona ambalo limeikamata dunia kwa sasa.
Sambamba na hilo, wanasoka kibao huko Ulaya wamekuwa akitoa michango mbalimbali ya pesa na vifaa tiba kuhakikisha wanapambana kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo vya Corona.
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola naye ametoa kiasi cha Euro 1 milioni kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Corona huko Catalunya, huku mchezaji kama Cristiano Ronaldo akikubali kukatwa mshahara wake karibu Pauni 3.5 milioni ili kusaidia kwenye vita hiyo kubwa ya dunia.