Tanzania kukata utepe Zambia ya Micho CHAN2020

Muktasari:

Mashindano ya Chan 2020 yanashirikisha timu za taifa za Mataifa 16 ambazo ni wenyeji Cameroon, Guinea, Togo, Morocco, Namibia, Libya, Niger, Congo, DR Congo, Zambia, Rwanda, Uganda, Mali, Burkina Faso, Zimbabwe na Tanzania.

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', imepangwa kukutana na Zambia katika mchezo wake wa kwanza wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) utakaochezwa Aprili 7 mwaka huu katika Uwanja wa Limbe nchini Cameroon.

Mechi hiyo itaanza mnamo saa 11.00 jioni kwa saa za Cameroon sawa na saa 1.00 usiku na itafuatiwa na mchezo mwingine wa kundi la D baina ya Guinea na Namibia.

Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo iliyotolewa leo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), viwanja vinne vilivyopo katika miji mitatu ya Douala, Limbe na Yaounde ndio vitakavyoandaa mechi za mashindano hayo yatakayoanza Aprili 4 hadi 25 mwaka huu.

Aprili 11, Stars itarudi tena uwanjani kukabiliana na Namibia ikiwa ni mechi yake ya pili ya hatua ya makundi ya mashindano hayo ambao utachezwa katika uwanja nhuohuo wa Limbe kuanzia saa 4.00 usiku kwa saa za Tanzania ukitanguliwa na mchezo baina ya Zambia na Guinea.

Stars itatupa karata yake ya mwisho ya hatua ya makundi katika mashindano hayo mnamo Aprili 15 kwa kuivaa Guinea katika mchezo uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Reunification jijini Douala kuanzia saa 4.00 usiku kwa muda wa Tanzania.

Mchezo wa ufunguzi wa kundi D baina ya Tanzania 'Taifa Stars' na Zambia katika fainali za Chan mwaka huu unakumbushia mechi baina ya timu hizo mbili katika fainali za mashindano hayo mwaka 2009 uliokuwa wa kundi A ambao ulimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa ni wa mwisho kwa upande wa kundi A uliochezwa Februari 29, 2009 jijini Bouake, Stars ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia mkwaju wa penalti ya nahodha Shadrack Nsajigwa katika dakika ya 88 lakini wakati kila mmoja akiamini Stars ingeibuka na ushindi katika mchezo huo, Dennis Banda aliisawazishia Zambia katika muda wa nyongeza na kuifanya Tanzania imalize ikiwa nafasi ya tatu na kushindiwa kutinga hatua ya nusu fainali.