Yanga yaja na sapraizi Kigamboni Sports Complex home of Champions

Muktasari:

Ujenzi wa mradi huo umepewa jina la ‘ Kigamboni Sports Complex home of Champions’ unaanza mwezi Juni mwaka huu na hasa baada ya kipindi cha mvua kumalizika ili kuepusha usumbufu.

YANGA wamefanya tathmini ya viwanja vyote vikubwa jijini Dar es Salaam ukiwemo ule wa Azam Complex na wametamka wanakuja na bonge la sapraizi kwa mashabiki wao.
Vigogo wa Yanga wamesisitiza hawakwenda kwenye viwanja hivyo kujifurahisha bali kusoma mazingira na kuyajumuisha wakiwa na wataalam wa hali ya juu kuhakikisha wanakuja na kitu cha tofauti kabisa pale Kigamboni.
Ujenzi wa mradi huo umepewa jina la ‘ Kigamboni Sports Complex home of Champions’ unaanza mwezi Juni mwaka huu na hasa baada ya kipindi cha mvua kumalizika ili kuepusha usumbufu.
Katibu Mkuu wa Kamati  ya Ujenzi na Miundombinu wa Yanga, Said Mrisho alisema; “Tunataka Yanga iwe klabu ya mfano ambao unaendana na hadhi ya jina lake. Ni klabu ambayo ina historia kubwa sana nchini, kwa hiyo hata wageni wakija kuitembelea, wawe wamekutana na kitu cha kihistoria na kwenda kusimulia huko waendako.”
Alifafanua uongozi wa Yanga umejipanga kuhakikisha mradi huo unaanza na kuwa na kasi kubwa ili kukamilika kwake. Mrisho pia alisema suala la bajeti na wapi klabu itapata fedha halina tatizo.
Awali walikuwa na mpango wa ujenzi wa uwanja wa mazoezi eneo la Jangwani (Kaunda), lakini waliamua kusitisha zoezi hilo kutokana na mradi mkubwa wa serikali ambao utafanyika katika eneo hilo.
Mrisho alisema wanaamini kuwepo  kwa mradi huo, klabu itafaidika nao kwani tatizo kubwa la mafuriko litakuwa limepatiwa ufumbuzi na wao kuanza mpango wa kujenga uwanja wa mazoezi eneo hilo ambao utatumika zaidi na timu ya vijana na ya wanawake.
Alisema kuwa mchoro wa uwanja wa Kigamboni umekamilika na utakuwa na viwanja viwili kimoja cha nyasi bandia na kingine cha nyasi za asili. Alisema kuwa viwanja vyote hivyo havitafanana na vya klabu nyingine ukiwemo ule wa Azam Complex ambao unaonekana wa kisasa na gharama zaidi nchini.
Kwa mujibu wa Mrisho kiwanja cha mazoezi kitakuwa na vifaa vya kisasa ikiwa pamoja na gym na Sauna.
Sambamba na hayo, pia kutakuwa na uwanja wa mpira wa kikapu, mpira wa wavu na bwawa la kuogelea la mita 50 linalokidhi viwango vya Kamati ya Olimpiki Duniani (IOC), Michezo ya Madola na Shirikisho la kuogelea duniani (Fina).
Alisema lengo la kujenga bwawa la kuogelea ni kuwawezesha waogeaji wa Tanzania kuweka kambi katika eneo hilo wakati wakijiandaa na mashindano ya kimataifa na kuepuka kwenda nje ya nchi kufanya mazoezi. Pia alisema uwanja wa mechi utakuwa na urefu kama  Uwanja wa Taifa na kuingiza watu wasiozidi 20,000.
Alisema uwanja huo mbali ya kuutumia kwa baadhi ya mechi ambazo hazina mashabiki wengi, pia utatumika kwa ajili ya mechi za kimataifa za timu za vijana na wanawake za Tanzania.
 Aliongeza pia kutakuwa na vyumba vinne vya kubadilishia na utakuwa na uwezo wa kutumika kwa mechi mbili kwa siku bila ya muingiliano wa vyumba hivyo.
Vile vile uwanja huo utakuwa na vyumba vya matibabu ambavyo pia vitatumia kwa kupimia wachezaji wanaohisiwa kutumia dawa za kusisimua misuli.
“Kwa kifupi, tumezingatia mahitaji ya Caf na Fifa katika uwanja wetu ambao unaanza kujengwa mwezi Juni na hasa baada ya kipindi cha mvua kuisha,” alisema Mrisho.

KAULI YA UONGOZI
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Frederick Mwakalebela alisema kwa sasa uongozi wao upo katika mchakato wa kukamilisha baadhi ya taratibu za mradi huo ambao ni mkubwa.
Alisema uundwaji wa kamati ya Ujenzi na Miundombinu uliofanywa na Kamati ya Utendaji kwa kuzingatia sifa za wajumbe wake na wengi ni ma-injinia.
“Yanga ina mpango mkubwa sana kuhusiana na miundombinu, ndiyo maana mpaka sasa tumekutana na wataalam mbalimbali kwa lengo la kujua wao walifanyaje na kufanikiwa kujenga miundombinu yao,
“Mbali ya miondombinu, pia lengo letu ni kuwashirikisha kimawazo ili kuweza kuibuka na uwanja wa kisasa zaidi wa mechi na mazoezi,” alisema Mwakalebela.
Alisema Kamati ya Utendaji haijafanya makosa kuwachagua wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni ma-injinia wenye uwazo na weledi mkubwa wa kazi zao. “Suala la michoro haina shida, kwa kamati yetu ni jambo dogo sana, wajumbe wamejipanga na hata katika masuala ya gharama za ujenzi, uongozi umejipanga ili kufanikisha,” alisema.