Mbelgiji Eymael awadhibiti Tshishimbi, Feitoto Yanga

Muktasari:

Nahodha Papy Tshishimbi kwa upande wake alisema anaona ugumu kutokana na ligi kusimama muda mrefu huku akiweka wazi kuwa kama itaendelea kusimama hadi mwezi Mei, basi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lichukue uamuzi wa kuifuta.

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael ni kama kawatega mastaa wake akiwemo Papy Tshishimbi na Feitoto kwa kuacha programu ambayo kama wakiterereka kidogo tu kila kitu kitajidhihirisha wakirejea uwanjani.
Mastaa wa timu hiyo wamefunguka kwamba, kwa namna kocha huyo alivyoacha programu ya mazoezi mchezaji ambaye ataitegea atakuja kuumbuka.
Kiungo wa timu hiyo, Fei Toto alisema hana wasiwasi na mazoezi ya kufanya mwenyewe kwa sababu kocha kamwachia mwongozo ambao atahitaji mrejesho watakapoanza kazi.
“Hatuwezi kukutana na ugumu kutokana na ligi kusimama, ni jambo la kawaida tu kwa sababu tumepewa programu za kufanya na kocha kabla hatujaachana naamini hiyo ndio itakayotuongoza na kurudi tukiwa fiti,” alisema.
“Kusimama kwa ligi kwa muda huo tunatakiwa kuchukulia kama timu imepewa mapumziko kupisha mashindano yoyote ya timu ya Taifa kwani sio wachezaji wote wanaenda, kuna wanaobaki nyumbani lakini tukikutana tunaendelea na mapambano,” alisema.
Fei Toto ambaye ameweka wazi programu yake ya mazoezi kuwa anafanya mara tatu kwa siku, aliongeza kuwa ugumu utawapata nyota ambao wanatega mazoeziniu na sio yeye.
Naye beki wa timu hiyo, Ally Sonso aliongeza kuwa programu walizoachiwa ndizo zitatoa nafasi za wachezaji kuanza kikosi cha kwanza kulingana na namna watakavyokuwa wamemkosha kocha siku watakaporudi kikosini.
“Mwalimu ana akili kubwa kutuhimiza kufanya mazoezi kwa kutuachia programu maalumu, anafahamu akili za wachezaji, hivyo hicho ndicho kitakuwa kipimo chetu kuona kama tumefanyia kazi maagizo yake,” alisema.
Sonso alisema, “kungekuwa na ugumu kama kila mchezaji angekuwa anajiamulia kitu cha kufanya hapo tungekuwa na changamoto, lakini kwa maelezo tuliyopewa tutarudi tukiwa pamoja kama wote tutakuwa tumeyafuata.”
Nahodha Papy Tshishimbi kwa upande wake alisema anaona ugumu kutokana na ligi kusimama muda mrefu huku akiweka wazi kuwa kama itaendelea kusimama hadi mwezi Mei, basi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lichukue uamuzi wa kuifuta.
“Hili ni janga la dunia linaumiza kila mmoja hasa kwa upande wetu tumesimamisha kazi tunayoitegemea, hatujaonana na familia zetu kutokana na kushindwa kusafiri, hivyo tutahitaji kukutana nazo na pia ligi ikiendelea huo mwezi Mei msimu mwingine tutaanza lini?” alihoji.
Kwa sasa michezo mbalimbali imesimamishwa dunia nzima ili kupisha juhudi za kimataifa za kupambana na ugonjwa wa corona.