Beki wa Coastal Union atajwa kubeba mikoba ya Wawa Simba

Muktasari:

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ndiye alipokea ripoti ya Sven akitaka asajiliwe wachezaji wasiopungua watano wakiwemo wazawa katika nafasi za beki ya kati, kiungo mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia na straika matata kuliko John Bocco na Meddie Kagere.

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amewakabidhi mabosi wake mapendekezo yake ya usajili ili kuimarisha kikosi na tayari kazi imeanza kufanyika japo kimyakimya, lakini ghafla imebainika beki mpya wa kati ambaye klabu inamfukuzia kwa muda mrefu amewatikisa kiaina.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ndiye alipokea ripoti ya Sven akitaka asajiliwe wachezaji wasiopungua watano wakiwemo wazawa katika nafasi za beki ya kati, kiungo mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia na straika matata kuliko John Bocco na Meddie Kagere.
Mwanaspoti imepenyezewa kwenye eneo la beki wa kati, Simba walimpigia hesabu beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto ambaye mazungumzo yamekwenda vizuri na kukubaliana, lakini tatizo linakuja kwa mabosi wake wa sasa, yaani Coastal ambao wanaonekana kukomaa.
“Tunakwenda kukamilisha dili hili la Mwamnyeto ambaye kwangu mpaka tulipofikia katika mazungumzo yetu msimu ujao atacheza Simba sidhani kama kunaweza kutokea jambo jingine tofauti na hilo, ingawa tunafahamu Yanga nao wamemfuata na wanamtaka,” alifichua mmoja wa vigogo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba (jina tunalo).
Hata hivyo, beki huyo amesema bado hajafanya uamuzi wa kutua Simba ama kwingineko na kusema hata kama Yanga wanamtaka wafuate taratibu tu kwa vile kiu yake kuona anacheza timu yoyote kubwa itakayokidhi mahitaji yake kimasilahi.
Mwamnyeto alisema ni kweli Simba na Yanga zinamtaka, lakini hawajakubaliana na klabu yoyote mpaka sasa kwa vile anabanwa na mkataba wake wa mwaka mmoja uliosalia kwa Wagosi wa Kaya na sio kweli kama amesaini mkataba na Simba kama inavyovumishwa.
“Bado nawasikilizia Simba na Yanga, kwani wote wamekuja na watakaokuwa tayari kunipatia kile ambacho nahitaji kwa maana ya maslahi mazuri nitakuwa tayari kujiunga na timu yao, kwani hakuna ambacho nahitaji zaidi ya pesa nzuri na kupata nafasi ya kucheza, ila taratibu zifuatwe,” alisema.
Licha ya Mwamnyeto kuipotezea Simba, lakini mtu wa karibu wa mchezaji huyo amefichua kuwa ameshasaini mkataba wa miaka mitatu, japo mwenyewe anafanya siri.
“Mie ndiye nilimpeleka Yanga kwa mara ya kwanza akiwa bado hana jina kubwa, ila walimkataa na kuniambia hawezi kucheza timu hiyo, nikamrudisha Coastal akafanya kazi kubwa msimu uliopita na huu Yanga wakarudi tena kutaka kumsajili wakati huo thamani yake ikiwa imepanda kutokana na kuongeza mkataba mwingine,” alisema mtu huyo wa karibuni.
“Tumezungumza na Mwamnyeto na ameniambia tayari ameshasaini Simba ila kuna taratibu zinakuja kufanywa hapo baadaye na ndio watamtangaza rasmi kuwa ni mchezaji wao kwa maana hiyo Yanga itakuwa ngumu tena kwao kumpata mchezaji huyu kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita,” alisema mtu huyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe kwa sababu za kiusalama.

MNGUTO AFUNGUKA
Mwenyekiti wa Coastal, Steven Mnguto alisema anafahamu mchezaji huyo amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na timu yao ambao utamalizika mara baada ya mwisho wa msimu ujao.
Mnguto alisema kama kuna timu itakuwa imemsaini Mwamnyeto kwa mkataba wowote ule watakuwa wamekosea kwani mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Coastal kwa maana hiyo kama kuna jambo hilo limefanyika litakuwa ni mikosa.