Muumini Mwinjuma adai kutapeliwa Dodoma

Muktasari:

Muumini alikuwa akijiandaa kuzindua bendi yake ya Shadai, uzinduzi ambao ulipangwa kufanyika Jumamosi ya Machi 28, 2020 mjini Dodoma.

Dar es Salaam.Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi, Mwinjuma Muumini amedai kutapeliwa fedha za kubandika mabango ya matangazo ya bendi yake.

Muumini alikuwa akijiandaa kuzindua bendi yake ya Shadai, uzinduzi ambao ulipangwa kufanyika Jumamosi ya Machi 28, 2020 mjini Dodoma.

Muumini alifika jijini Dodoma Machi 14 kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi huo na ndipo alipotafuta watu wa kumsaidia kubandika matangazo sehemu mbalimbali.

Katika harakati hizo, Muumini alidai kukutana na mama mmoja aliyemtaja kwa jina la Mama Akudo ili kumsaidia katika kupata watu wa kubandika matangazo hayo.

Akielezea tukio zima lilivyokuwa Muumini alisema, "Unajua hii ishu sio hata ya kuandika maana nitaonekana kama mshamba vile, ila ki ukweli sijapenda na sijafurahishwa na tukio hili.

"Ishu iko hivi kwa ufupi, nilikutana na Mama Akudo Dodoma, katika maongezi ya hapa na pale nikazungumzia ishu ya uzinduzi wa bendi yangu, sasa ilikuwa jinsi ya kutaka watu wa kunibandikia matangazo ya uzinduzi, Mama akasema anawafahamu watu akanitafutia hao watu wa kubandika matambala ya matangazo.

"Aliniambia ana watu wa chama anawafahamu, wanabandikaga bendera za chama huwa wanatembea na pikipiki kubandika, nikaingia mashaka kidogo alivyosema watatembea na pikipiki, maana utatembeaje Sasa kubandika matambala na postaz mji mzima? na postaz zipo kama 500?  lakini nikaona  kukubali tu ndipo tukakubaliana kila mtu atapewa 10, akamleta mtu wa pikipiki kwanza, akachukua postaz 10 na kitambaa kimoja, nikampa 10 akaondoka zake, akaja mwingine anayeitwa Moses naye alikuja na pikipiki Mama Akudo alimpigia simu tukaelewana akaondoka kwenda kufanya kazi hiyo akiwa na vijana wake.

"Baada ya muda Moses akarudi akaniambia vijana wamemaliza kazi wamechoka njaa inawauma, akanionyesha na picha ya sehemu walizobandika matangazo, nikaona matambalaa sehemu nyingi yamebandikwa kupitia picha alizonionyesha kwa simu, hapo nikaingia uhakika nikatoa 37, kabla ya kuondoka nikasema nizurure na pikipiki ili kuona matangazo yaliyobandikwa mbali na kuona kwenye picha, ndipo nikapita majengo, Sokoni na sehemu nyingine tulizokubaliana, nikaona hakuna matangazo yoyote, nikasema hapa nimeingizwa chaka yaani hata Dodoma mjini hakuna tangazo lolote, ndipo nilipoamua kumpigia simu Mama Akudo ambaye ameniunganisha na hao watu , akaniambia nimpigie  Moses kumuuliza nikampigia akasema anakuja ila hana mafuta kwenye pikipiki yake, nikamwambia nitakulipa mafuta njoo."

Akifafanua zaidi Muumini alisema, "Moses akaja nikamwambia anizurulishe sehemu zote walizobandika matangazo vijana wake, akaniambia  anawapigia simu hawapokei kawatumia meseji hawajibu ila anajua matangazo sehemu yalipo, nikamwambia nipeleke nikayaone tumeenda hiyo sehemu tulipofika akaingia ndani  kutoa matangazo, yaani huwezi amini katika 500 yamebandikwa matangazo matano tu, na sehemu yaliyobandikwa ni Chako Ni Chako na hapo ni karibu na gesti niliyofikia, kiukweli nilipagawa nikachanganyikiwa, nikasema  potelea pote nipate hasara Mara mbili na ni bora nimeyapata hayo matangazo.

"Baada ya kuyachukua matangazo yangu, nikamwambia Moses umesema hawa huwapati kwenye simu Sasa umejuaje kama matangazo yapo hapa na ukaja kuchukua pesa kusema wamemaliza kazi wamechoka wanataka pesa, Sasa kazi haijafanyika naomba nirudishie hizo pesa, akasema alishawapa pesa hivyo yeye hana.

"Mimi nikaachana naye kwani sikutaka malumbano kuhusu hizo pesa, nilichofanya nikatoa pesa tena kwa watu wengine na kufanikisha zoezi hilo na hadi naondoka Dodoma matangazo yalikuwa yamebandikwa kila sehemu kwa ajili ya uzinduzi wa Machi 28, sema hautafanyika tena sababu ya zuio la Serikali kuhusu mkusanyiko wa ugonjwa wa virusi vya corona, najiandaa kwa tarehe nyingine nitatangaza

Mwanaspoti halikuishia hapo, lilimtafuta Mama Akudo ili aweze kuweka wazi suala hili na baada ya kupatikana alisema ni kweli tukio limetokea, na alimuunganisha Muumini na huyo Moses ambaye alimuamini lakini amefanya vitu ambavyo sivyo na kujiondoa uaminifu kwake.

"Hiyo ishu ni kweli kabisa imetokea,na sio kitendo kizuri kilichofanyika na kinatakiwa kikemewe ili hata watu wengine wawe waaminifu kwenye jambo hili, huyo Moses mimi namfahamu huwa anafanya kazi za chama, nilipomueleza hilo akatuletea watu wanaobandika bendera za chama akasema watakuwa wanajua maeneo yote,baada ya kumkabidhi mabango mimi na Muumini tulikaa sehemu tukiwasubiria, mara Moses akaja na mvulana mmoja akataka pesa kwa Muumini akapewa Elfu thelathini na saba, tulipoachana na Muumini, mimi sasa napopita barabarani sikuwa naona mabango nikamwambia Muumini mbona sioni mabango?,ndipo Muumini alipofanya mawasiliano na Moses wakaja sehemu niliyopo wakiwa na mabango, ikabidi nimwambie Muumini nitoe hela yangu kidogo ili mabango yakabandikwe tena maana Moses ndio kaharibu kazi yake na mimi sikutegemea kumuangusha, mabango yakabandikwa upya hadi anaondoka yalikuwa yashabandikwa alitumia watu wengine,'' alisema Mama Akudo.