Msuva aonya mapema kuhusu VAR

Monday February 10 2020
Msuvapic

STAA wa Difaa El Jadida ya Morocco, Saimon Msuva ‘Msuvan27’ ametoa tahadhali mapema kwa viongozi na wadau wa soka la Afrika ambao wako katika mchakato wa mwisho kuhakikisha teknolojia ya usaidizi kwa marefa (VAR)   inaanza kutumika katika michezo ya ligi za ndani.
Miongoni mwa mataifa ambayo yapo katika mchakato huo ni Morocco anakocheza soka la kulipwa na Misri ambako wamekuwa na semina za hapa na pale zenye lengo la kuwanoa waamuzi juu ya namna ya kutumia teknolojia hiyo.
Msuva alisema viongozi wanatakiwa kuingia katika matumizi ya VAR kikamilifu na sio kujaribisha, vinginevyo wanaweza kuharibu badala ya kutatua changamoto za kimaamuzi.
“Inaweza kuwa kituko kama muda ambao inatakiwa kuangalia utata wa tukio halafu unakuta kumbe mitambo ilizimika, uzuri Waafrika tunajijua tulivyo, lazima patachimbika, kwa hiyo wito wangu ni bora tuchelewe kutuma VAR ili tuanzie pazuri,” alisema.
Msuva aliongeza kwa kusema kuwa Wazungu  wenye teknolojia yao bado inawasumbua. “Nina wasiwasi kuwa badala ya kutibu tatizo tusije kuongeza matatizo, maana Ulaya kwenyewe kila siku kumekuwa na malalamiko ya VAR, ngoja tuone lakini.”
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Morocco, VAR huenda ikaanza kutumika nchini humo msimu ujao wa 2020/21, huku kwa upande wa Misri wakiwa katika mchakato wa kuwaweka sawa waamuzi kabla ya kufikia uamuzi wa kuanza kutumia teknolojia hiyo.
Mnamo Mei 31, mwaka jana, mchezo wa pili wa marudiano wa hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Esperance na Wydad Casablanca ulivunjika kutokana na VAR.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Olimpiki uliopo Rades huko Tunisia, ilivunjika baada ya Wydad Casablanca kugoma kuendelea kucheza wakipinga uamuzi wa refa Bakary Gassama kutoka Gambia ambaye alikataa bao lao la kusawazisha  katika dakika ya 58 lililofungwa na Walid El Karti.
Bao hilo lilikataliwa kwa kile kilichodaiwa kuwa kulikuwa na mchezaji aliyeotea ambaye aliingilia mchezo.
Mara baada ya kukataliwa bao hilo, wachezaji wa Wydad Casablanca waligoma wakimtaka mwamuzi Gassama kwenda kutazama marudio kupitia teknolojia ya video (VAR) ambayo hata hivyo baadaye ilionekana imeharibika na haiwezi kufanya kazi.
Hadi sasa hakuna ligi yoyote barani Afrika ambayo inatumia VAR.

Advertisement