Mkude v Stars, Morrison v Simba, Luis v Morrison walishika kila kona kabla ya corona

Thursday March 26 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Mkude v Stars, Morrison v Simba, Luis v Morrison walishika kila kona kabla ya corona

 

By OLIPA ASSA

KABLA ya tangazo la serikali kusimamisha shughuli za mikusanyiko ya watu, lengo likiwa ni kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona kuna mambo yalibamba Ligi Kuu Bara.
Mashabiki walitumia muda wao kuyajadili hayo, baadhi wakipata majibu yake na mengine yakiendelea kuacha maswali mioyoni mwao.
Mwanaspoti limekukusanyia mambo ambayo kabla ya Corona kuzungumzwa kila kona, yenyewe ndio yalikuwa habari ya mjini.

MKUDE VS STARS
Kitendo cha kiungo wa Simba, Jonas Mkude kushindwa kujiunga na Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na michuano ya Chan 2020, kilizua sintofahamu zaidi pale kocha wake Etienne Ndayiragije na meneja kutokuwa na taarifa zake.
Ikaonekana mchezaji huyo ni tabia yake ya utovu wa nidhamu, lakini baadaye akalitolea ufafanuzi jambo hilo kwamba viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wana taarifa nalo.
“Naonekana sina nidhamu lakini ifahamike kwamba hakuna mchezaji ambaye hapendi kuitumikia timu yake ya Taifa, viongozi walikuwa na taarifa yangu,” kauli ya Mkude.
Baada ya kutoka mafichoni ni kama Mkude alibadilisha upepo wa kumhusisha na Taifa Stars kisha kuzungumzi wa historia yake ya alipotoka, akitaja na waliomshika mkono akiwemo kocha wake msaidizi Seleman Matola.

MORRISON VS SIMBA
Mashabiki wa Simba ndio wanajua uhalisia wa maumivu waliyoyapata dhidi ya staa wa Yanga, Bernard Morrison ambaye aliwatungua kwa bonge la bao la frii-kiki kwenye kipigo cha 1-0 katika mechi ya watani wa jadi.
Habari ya mjini akawa Morrison kwa namna alivyojitambulisha mbele ya mashabiki wake wake akitumia vionjo vya mbwembwe za shibobo akitembea juu ya mpira na kupiga pasi kwa madaha.
Wafuasi wa Yanga walimtumia BM33 kama fimbo ya kuwachapia Simba kwa kejeli mtaani na kuwafanya Wekundu wa Msimbazi kujiona wanyonge licha ya kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi.

LUIS VS MORRISON
Simba na Yanga ni asili yao kushindana kuanzia uwanjani hadi kwenye usajili wao. Msimu huu nyota zimeng’ara kwa Morrison na Luis Miquissone ambao uwezo wao unawakosha wadau.
Kama sio ubabe wa Corona, majina ya hawa jamaa yangeongoza kwa kutajwa zaidi nchini katika soka la Bongo.

HAT-TRICK YA KAGERE
Amekuwa aking’ara na kupotea. Kabla ya ligi kusimamishwa aliacha alama ya kukumbukwa kwa wafuasi wa Simba.
Kagere ndiye kinara wa mabao 19 kwenye msimamo wa wafungaji, alifunga mabao manne, Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Singida United, ukiwa mchezo wa pili baada ya kutoka kufungwa 1-0 na Yanga.

WAZAWA WALIONG’ARA
Kuna wazawa ambao walifanya vyema kwenye ligi hususani upande wa wafungaji kama Yusuf Mhilu kutoka Kagera Sugar ana mabao 11.
Wengine ni Paul wa Lipuli (ana mabao 11), Reliants Lusajo wa Namungo FC naye ana miliki mabao 11 na Peter Mapunda wa Mbeya City mabao tisa, hao ni baadhi tu.

MORRISON, MKUDE DHIDI YA TFF
Kabla ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga kilichokuwa kinawapasua kichwa mashabiki ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutakiwa kuwachukulia hatua, Jonas Mkude na Bernard Morrison.
Ilikuwa inawashangaza wadau kuona kamati za TFF zikijizungushazungusha tu bila ya kutoa adhabu kwa nyota hao ambao walifanya vitendo visivyo vya kiungwana, hadi mechi hiyo ikapita.

Advertisement