Kijiwe cha Salim Said Salim: Ronaldo, Pele, Cruyff na imani za ushirikina

Thursday March 26 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Kijiwe Ronaldo, Pele, Cruyff na imani za Corona, ushirikina

 

By Salim Said Salim

Katika nchi nyingi siku hizi badala ya mafunzo, mazoezi na lishe bora kuwa siri ya mafaniko katika kandanda, ushirikina unapewa umuhimu na klabu, wachezaji na mashabiki.
Ukielezewa mambo ya baadhi ya wachezaji, wakiwemo maarufu duniani wanayoyafanya kwa kuamini yatawasaidia kucheza vizuri na timu zao kushinda hutaamini.
Tafiti zinaonyesha wapo wachezaji walioamua kutokana na imani kwamba wakivaa chupi siku zote wanapoingia uwanjani watashinda na wakibadili matokeo hayatakuwa mazuri. Kwa muhtasari nimeona nieleze imani hizi au ushirikina wa aina moja au nyingine wa makocha na wachezaji wachache mashuhuri.
Nianze na Mario Zagallo, kocha wa zamani wa Brazil iliyokuwa na wachezaji mahiri kama Pele, Jairzinho na Tostao ambaye alikuwa tafauti na walimu wengi wa soka wa Ulaya na Amerika Kusini juu ya jezi namba 13.
Wakati wenzake waliiona  namba 13 ni mkosi yeye aliiona ni ya bahati na alilazimisha kutumika katika timu yake.
Kocha wa zamani wa Ufaransa, Raymond Domenech mara nyingi na wakati wa Fainali za Kombe la Dunia za 2010 alishirikiana na mchawi kupanga timu na kusema  alikuwa ni mchezaji wake wa 12.
Carlos Bilardo, aliyekuwa kocha wa Argentina alikuwa akilazimisha wachezaji
 kwenda uwanjani na taksi kwa kuamini ukipanda basi wakati ukiwa na mchezo huenda hilo limefanyiwa mambo ya juju. Alisema taksi zilikuwa na bahati ya aina yake kwa timu ya Ufaransa.
Mchezaji maarufu na baadaye kocha, Johan Cruyff wa Uholanzi, alikuwa kabla ya kuingia uwanjani anampiga ngumi ya nguvu mlinda mlango wake Fabian Bartez na kuhakikisha anatema mate upande wa wapinzani kama tambiko la kupata ushindi.
Cristiano Ronaldo wa Ureno anayeichezea Juventus ya Italia akipanda basi na wachezaji wenzake wanapokwenda uwanjani hukaa kiti cha nyuma, akipanda ndege hukaa kiti cha mbele na anapoingia uwanjani huanza na mguu wa kulia.
Johnny Warren, mchezaji wa zamani wa Australia alikiri mara nyingi kuamini ushirikina. Mara moja katika mwaka 1969 wakati wa kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Mexico alikwenda Msumbiji kupata msaada wa mganga.
Huko alipewa mifupa aliyoizika pembezoni mwa goli la wapinzani na aliamini hiyo mifupa iliwasaidia kupata ushindi.
Kolo Toure wa Ivory Coast aliamini nafasi ya kushinda mchezo huwa kubwa kama anakuwa mchezaji wa mwisho kuingia uwanjani.
Nahodha wa zamani wa Uingereza, John Terry, alieleza yapo mambo aliyoyafanya kabla ya mchezo akiamini yalimsaida na timu yake kushinda.
Miongoni mwao ni kuweka gari yake sehemu hiyohiyo walipocheza uwanja wa nyumbani na alimtuma mtu saa kadhaa kabla ya mchezo kuhakikisha nafasi hiyo ya kuegesha gari ilimsubiri.
Kocha wa Ufaransa, Laurent Blanc aliamini upara wa kipa Fabien Barthez ulileta baraka na ushindi alipoubusu kabla ya mchezo. Hilo alilifanya hadharani na liliwachekesha watazamaji wakati wa michezo ya Fainali za Kombe la Dunia za 1998 ambapo Ufaransa ilibeba kombe.
Mara nyingi alipendelea wake wa wachezaji au marafiki zao wawabusu wapenzi wao kabla ya kuingia uwanjani.
Naye mfalme wa soka duniani Pele (jina lake ni Edson Arantes do Nascimento) alikuwa na mambo yake.
Katikati ya miaka ya 1960 Pele alipoteza ustadi na uwezo wa kufunga mabao. Hali hii ilifanya mashabiki kumwambia muda wake wa kung’ara ulifikia kikomo na alikuwa mzigo usiobebeka kwa wenzake.
Alipotafakari kwa nini hachezi vizuri, Pele aliamini kutokuwa na shati lake la zamani ambalo lilikuwa na bahati naye ndio sababu.
Hilo shati alilolivaa alipoichezea klabu ya Santos alimpa kama zawadi shabiki mmoja wa klabu hiyo.
Kutokana na imani hiyo, Pele alimkodi kachero kumtafuta shabiki aliyempa lile shati amrudishie. Kachero alihangaika kumtafuta aliyekuwa na shati na hakumpata, lakini
hakutaka kumuumiza Pele. Alitafuta shati lililofanana na lile alilolitaka Pele na kumpa.
Kutoka pale kiwango cha Pele kilipanda na kuamini  ilitokana na bahati ya lile shati la zamani.
Pele alijua kama miaka sita iliyopita kwamba yule kachero alimpiga chenga ya mwili kama alivyowafanyia wachezaji wa timu alizocheza nazo.
Mpaka leo Pele licha ya kustaafu na akiwa mgonjwa bado anamuulizia mtu au familia yenye lile shati la bahati kwa kuamini litampatia bahati zaidi.
Malvin Kamara aliyechezea klabu za MK Dons, Cardiff City, PortVale, Huddersfield na Grimsby za England kabla ya kwenda uwanjani aliangalia mchezo wa Sienna wa 1971 Willy Wonka & The Chocolate Factory (Willy Wonka na kiwanda cha kutengezea chokoleti).
Upo msemo maarufu wa kwamba magolikipa wengi ni vichaa. Mlinda mlango wa zamani wa Argentina, Sergio Goycochea, naye alikuwa na yake ya ushirikina.
Kila ilipotokea kupigiwa penalti alijikojolea kwa kuamini kufanya hivyo kulimsaidia kuzuia mpira usitikise nyavu.
Katika msimu wa 1992-93 mshambuliaji wa Sheffield United, Alan Cork, aliamua asinyoe ndevu tokea mwanzo hadi mwisho wa mashindano ya Kombe la FA.
Aliamini hiyo ilimsaidia kuiwezesha klabu yake kufika fainali na ilishindwa kubeba kombe baada ya kocha wake kumlazimisha kuzinyoa.
Mchezaji maarufu wa zamani wa Ajax ya Uholanzi, Johan Cruyff, aliamini anapompiga ngumi ya tumbo golikipa wake Gert Bals dakika chache kabla ya kuingia uwanjani husaidia kuwapatia ushindi.
Akimaliza hilo huingia upande wa wapinzani kabla mchezo kuanza na kutema ubani aliokuwa anautafuna kwa kuamini ungewapumbaza wapinzani.
 

Advertisement