Horoya yawaita Yanga mezani kujadili hatma ya Makambo

Muktasari:

Kuondoka ama kutoondoka kwake kutategemea na ofa ambayo Yanga itakuja nayo maana sisi kama Horoya kwa sasa hatuna mpango wa kumuona anaondoka kwenye timu, kwani ni mmoja kati ya wachezaji wetu muhimu

HOROYA AC ya Guinea imesisitiza kwamba bado haijapata ofa yoyote ya Yanga kuhusiana na mchezaji wao, Heritier Makambo.
Mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na kurejea Yanga ingawa viongozi hawajataka kuweka wazi kwa madai kwamba muda bado.
Ofisa Habari wa Horoya, Elhadj Ibrahima Kalil ameliambia Mwanaspoti kuwa, “tunachojua ni kwamba Makambo bado ana mkataba mrefu na sisi na bado hatuna mpango wa kutaka kumuacha, ikiwa Yanga watawasilisha ofa yoyote basi tutatoa taarifa hiyo ila kwa sasa hatujawasiliana chochote na Yanga kuhusu mchezaji huyo,” alisema.
“Kuondoka ama kutoondoka kwake kutategemea na ofa ambayo Yanga itakuja nayo maana sisi kama Horoya kwa sasa hatuna mpango wa kumuona anaondoka kwenye timu, kwani ni mmoja kati ya wachezaji wetu muhimu amekuwa na msaada mkubwa kwenye michuano ya kimataifa na hapa ambapo tumefikia juhudi zake zimechangia sana.
“Ninachoweza kusema mpaka sasa hakuna ofa tuliyopokea kutoka kwa Yanga, hayo yanayoendelea huko Tanzania ni uvumi tu ambao hauna ukweli wowote, ikiwa Yanga wataleta ofa yoyote basi tutaweka bayana lakini mimi kama mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa Horoya AC nathibitisha kuwa hakuna jambo kama hilo.”
Makambo aliiambia Mwanaspoti wiki hii kwamba hajapata ofa ya Yanga, lakini wadhamini wa klabu hiyo, GSM, walisisitiza kwamba kama viongozi wakipeleka ishu hiyo mezani wataangalia linalowezekana.