Mapinduzi Balama ataja siri yake Yanga

Kiungo wa Yanga, Mapinduzi Barama (kushoto) akimpiga chenga kiungo wa Tanzania Prisons, Adilly Buha katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliofanyika Jumamosi Februari 15, 2020.Timu hizo hazikufungana. PICHA NA MICHAEL MATEMANGA

Muktasari:

Ameonyesha maajabu makubwa kwani tangu amejiunga kwenye timu hiyo, amekosa kucheza mechi tatu tu za Ligi Kuu Bara kati ya 19 walizokwishacheza (kabla ya mchezo wa jana na Tanzania Prisons).

TANGU ajiunge na Yanga, Mapinduzi Balama amekuwa hakamatiki na mchezaji yeyote ndani ya kikosi hicho kwani ndiye kinara wa kucheza mechi nyingi jambo alilosisitiza ni kwa sababu ya nidhamu na kujituma.
Mapinduzi ambaye ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji wa kati na pembeni, alisajiliwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Alliance FC ya Mwanza.
Ameonyesha maajabu makubwa kwani tangu amejiunga kwenye timu hiyo, amekosa kucheza mechi tatu tu za Ligi Kuu Bara kati ya 19 walizokwishacheza (kabla ya mchezo wa jana na Tanzania Prisons).
Mechi alizoshindwa kucheza Mapinduzi ni dhidi ya Tanzania Prisons, Mbeya City zilizopigwa Mbeya pamoja na Alliance FC na mchezaji huyo aliweka wazi ni kwa sababu alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya enka ya mguu wa kulia.
“Nafikiri ni makocha wenyewe kuna kitu wanakiona kwangu, lakini kubwa ni kwa sababu najituma, nidhamu na ushirikiano mbele ya wachezaji wenzangu,” alisema Mapinduzi.
Meneja wa Yanga, Abeid Mziba amesema Mapinduzi ndiye mchezaji aliyecheza idadi kubwa ya mechi.
“Tangu niingie kwenye majukumu yangu ya kazi Yanga, Mapinduzi ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi ya mechi,”alisema Mziba ambaye enzi zake Yanga ilimsajili kwa Sh9000 tu.