Sven uso kwa uso na mbaya wa Simba akiwa Stand United

Muktasari:

Simba inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 62, huku Stand United wakiwa na alama 16 katika nafasi ya 10 kwenye kundi lao B linaloongozwa na Gwambina wenye 31 baada ya mechi 15.

Mwanza. Achana na kasi ya Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sven Vanderbroek kesho Jumanne atakuwa na kibarua kizito mbele ya Stand United.

Simba imewasili leo asubuhi mjini Shinyanga tayari kuwakabili Stand United katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaopigwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage.

Simba chini ya Mbelgiji Sven watakuwa na kazi ngumu kwani wanaenda kukutana na Kocha Atuga Manyundo aliyewafunga msimu uliopita na kuwaondoa kwenye michuano hiyo hatua ya 32.

Katika msimu huo, Manyundo alikuwa akiiongoza Mashujaa FC ambaye aliitungua Simba mabao 3-2, mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiwa chini ya Patrick Aussems na sasa wanakutana tena akiwa na kikosi cha Stand United.

Hata hivyo Simba inakutana na Stand United ikijivunia rekodi ya ushindi katika dimba hilo, kwani mara ya mwisho kukutana na timu hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita walishinda bao 1-0 kabla ya kushuka daraja.

Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi 62, huku Stand United wakiwa na alama 16 katika nafasi ya 10 kwenye kundi lao B linaloongozwa na Gwambina wenye 31 baada ya mechi 15.

Sven alisema wanaenda kuwakabili wapinzani hao bila kujali historia ya nyuma, isipokuwa kwa sasa timu hiyo inaheshimu kila mechi.

Alisema amewaandaa vyema wachezaji wake na anaamini watafanya vizuri kwani malengo yao ni kufika mbali kwenye michuano hiyo na kwamba hawajui wapinzani hivyo wanaenda kupambana.

“Hatuchezi kwa rekodi na sitaki kufikiria yaliyotokea nyuma, tunawaheshimu wapinzani na tunaenda kupambana kuhakikisha tunashinda, vijana wangu wako fiti” alisema Vanderbroek.

Kocha Mkuu wa Stand United, Manyundo alisema mbinu alizotumia msimu uliopita kuwaondosha, ndio hizo hizo zitatumika leo na kutamba kuwa vijana wana ari na morari.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu kucheza na Simba yenye wachezaji kama Kagere, Kahata, Wawa, Mkude na Dilunga lazima ujipange, kwahiyo sisi tuko vizuri na mbinu zangu ni zilezile” alitamba Manyundo.