Simbu, Failuna kutumia laki tatu kwa siku kwa miezi minne kambini Kenya

Muktasari:

Simbu na Failuna watachuana katika mbio za marathoni (kilomita 42) kwenye Olimpiki ya msimu huu itakayoanza Julai 26 jijini Tokyo.

Dar es Salaam.Wanariadha, Alphonce Simbu na Failuna Abdi wataingia kambini Machi Mosi kujiandaa na maandalizi ya Olimpiki 2020 kwa gharama ya euro 128 kwa siku (sawa na Sh 319,748 za Tanzania) kwa miezi minne na wiki tatu katika mji wa Iten nchi Kenya.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka alisema kambi hiyo itafanyika kwa miezi minne na wiki tatu kabla ya wachezaji hao kwenda Japan kwenye Olimpiki.

Alisema maandalizi yote ya kambi yamekamilika ikuwamo wanariadha kuridhia kuanza kambi hiyo kwa maandishi.

Alisema wanariadha wengine watakaofikia viwango watajumuishwa katika kambi hiyo moja kwa moja baada ya kuthibitika rasmi kuwa wamefuzu.

"Tunahitaji kufanya mazoezi kwa kiwango bora, wanariadha wetu watakuwa kule na tutakuwa na utaratibu wa kuitembelea kambi hiyo sanjari na familia zao," alisema Mtaka.