Niyonzima kazaliwa upya, Yanga ikimkosa majanga

Muktasari:

Eymael, alisema kiungo huyo alikosa pambano hilo kwa kuugua Malaria na kumvurugia mipango yake kwenye mchezo huo wa juzi ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa, ingawa ana matumaini ya kumtumia mechi yao ya kesho dhidi ya Polisi Tanzania.

MASHABIKI wa Yanga wanasonya sana. Baada ya chama lao juzi Jumamosi usiku kushindwa kuendeleza ubabe mbele ya Tanzania Prisons, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael amekiri pengo la kiungo fundi wa mpira, Haruna Niyonzima ndilo lililowaangusha na hata sare ni bahati kwao.
Mbelgiji huyo alisema, Niyonzima (pichani) ni mmoja kati ya wachezaji ambao wanajua kuiendesha timu na katika mchezo wa juzi, Yanga ilicheza kawaida sana kutokana na kuzidiwa na wapinzani wao.
Eymael, alisema kiungo huyo alikosa pambano hilo kwa kuugua Malaria na kumvurugia mipango yake kwenye mchezo huo wa juzi ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa, ingawa ana matumaini ya kumtumia mechi yao ya kesho dhidi ya Polisi Tanzania.
Kocha huyo alisema kwenye mchezo huo ambao staa wao, Mghana Bernald Morrison alipaisha penalti, Niyonzima angekuwepo angeharibu mipango mingi ya wapinzani wake kutokana na aina ya uchezaji wake.
“Haruna (Niyonzima) ni mchezaji ambaye anazunguka sehemu zote katikati inakuwa rahisi kusaidia timu na kuvuruga mipango ya maadui mchezoni, ninachoamini kama angekuwepo kungekuwa na jambo,” alisema Eymael.
Kiungo huyo aliyerejeshwa Jangwani akitokea AS Kigali ya kwao, Rwanda alikoenda kuichezea baada ya kutemwa na Simba iliyomsajili misimu miwili akitokea Yanga, amekuwa mmoja kati ya nyota tegemeo ndani ya kikosi hicho, akishirikiana na wachezaji wengine waliosajiliwa msimu huu.
“Natarajia tutakuwa naye kwenye safari ya Moshi kucheza na Polisi Tanzania. Tunatarajia kuondoka Alfajiri kesho (jana) tayari kwa mchezo huo.”

YIKPE MIPANGO YAKE
Mbali na Niyonzima aliyekuwa anaumwa na nafasi yake kuchezwa na Mohammed Issa ‘Banka’ kwenye kikosi cha kwanza alikuwa anawaanzisha, aliwapumzisha wengine wanne na kufanya idadi kuwa watano na  Eymael alisema ni mipango yake.
Alimpumzisha, Jafary Mohammed kwenye beki ya kushoto akidai ni uchovu, nafasi yake ilichezwa na Adeyum Saleh, kipa Metacha Mnata kwa Mkenya Farouk Shikalo.
Pia, safu ya ushambuliaji aliwaweka pembeni Ditram Nchimbi  aliyekuwa akitumikia kadi tatu za njano, David Molinga akawaanzisha Muivory Coast  Yikpe Gnamien na Tariq Seif. Lakini, kipindi cha pili aliwatoa Yikpe na Tariq akawaingiza Molinga na Mrisho Ngassa.

PRISONS WALIPANIA
Katika hatua nyingine, nahodha na beki wa Tanzania Prisons, Laurian Mpalile alifichua waliamua kuwafanyia kweli Yanga kwenye mchezo huo ulioisha kwa suluhu kwa kuepuka kejeli wanazopewa kwamba wanaiachia sana Yanga.
Mpalile anayecheza beki ya kushoto alisema, baada ya kufungwa mechi mfulizo na Yanga kama FA Uwanja wa Taifa mabao 2-0 na mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi Kuu Bara 1-0 uliopigwa Uwanja wa Samora, wadau wengi waliwakejeli wamekuwa wateja wa Yanga, hivyo wakaamua kupambana.
“Lengo letu kabisa msimu huu ni kuona tunaifunga Yanga hapa Dar es Salaam lakini hata hiyo, sare kwetu sawa tu kwa sababu tumegawana pointi,” alisisitiza Mpalile.
Alisema hata kile kitendo cha mshambuliaji wa Yanga, Mghana Bernald Morrison kutembea juu ya mpira kwenye mechi yao ya FA kiliwaumiza.
“Umeona mchezo uliopita Yanga walitamba mno hadi Morrison akatembea juu ya mpira, lakini tulisema safari hii hatukubali na kikatokea tulichopata,”alifafanua Mpalile. Katika mchezo huo, Morrison alicheza kwa kiwango cha juu na kuisababishia timu yake kupata penalti lakini aliipiga  kuipaisha na mchezo kuisha kwa suluhu.