Matola: Ndemla anakipaji ila sina uwezo wa kumpanga Simba SC

Muktasari:

Matola alisema Ndemla ni mchezaji mwenye kipaji sio wa kufundishwa, hivyo pamoja na kukosa nafasi ya kucheza ndani ya Simba akipata nafasi anaweza kucheza vizuri na kuwazidi nyota wanaopata nafasi.

KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola ametamka kwamba hana mamlaka ya moja kwa moja ya kumuingiza kwenye kikosi cha kwanza staa anayedodea benchi, Said Ndemla.
Matola ambaye aliwahi kuwa nahodha wa Simba alisema labda mchezaji huyo haingii kwenye mfumo wa kocha mkuu.
Ndemla alianza kuitumikia Simba baada ya kupandishwa kutoka kikosi B mwaka 2013 na kucheza kwenye mchezo wa watani Simba na Yanga mechi iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 chini ya Kocha Patrick Liewig.
Matola alisema Ndemla ni mchezaji mwenye kipaji sio wa kufundishwa, hivyo pamoja na kukosa nafasi ya kucheza ndani ya Simba akipata nafasi anaweza kucheza vizuri na kuwazidi nyota wanaopata nafasi.
“Kuhusu kutolewa kwa mkopo ni jukumu la mchezaji mwenyewe na uongozi wa timu anayoichezea, mimi siwezi kulizungumzia sana kikubwa ninachoamini ni kwamba ni mchezaji mzuri na bora kama akipewa nafasi ya kucheza mara kwa mara,” anasema. “Nimemfundisha Ndemla, namfahamu vizuri na mimi ndiye niliyeushawishi uongozi umpandishe sambamba na Willium Lucian ambaye sasa anacheza Polisi Tanzania ni zao langu hilo nikiwa kocha msaidizi Simba.”
“Kakosa nafasi Simba huenda ni kutokana na kutoendana na mfumo wa mwalimu, mimi ni msaidizi tu sina nafasi ya kulazimisha nani apangwe na nani aachwe, kuhusu kumshauri aondoke akajaribu maisha sehemu nyingine hili nalo lipo ndani ya uwezo wake,” anasema Matola ambaye ni staa wa zamani wa Simba na Supersport ya Afrika Kusini.
Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema: “Ninachoweza kuzungumza ni kwamba ni mchezaji asiyejitambua ndio sababu ya kushindwa kutambua kipaji chake na kukifanyia kazi kwani kukosa kwake namba Simba haoni kama changamoto ameridhika kukaa benchi na kuua kipaji kikubwa alichonacho.”