Katibu Mkuu CAF afariki dunia kwa ugonjwa wa saratani

Muktasari:

Amr Fahmy alikuwa Katibu Mkuu wa CAF kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2019 alipotimuliwa baada ya kumtuhumu Rais wa shirikisho hilo, Ahmad Ahmad kujihusisha na masuala ya rushwa na ubadhilifu wa fedha.

Dar es Salaam.Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Amr Fahmy amefariki dunia jana nchini Misri kutokana na matatizo ya saratani yaliyokuwa yakimkabili.

Fahmy amekutwa na umauti ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu alipotimuliwa katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa CAF, baada ya kuvujisha taarifa za kumtuhumu Rais wa Shirikisho hilo, Ahmad Ahmad kujihusisha na rushwa na ufujaji wa fedha za maendeleo ya miradi ya mpira wa miguu.

Mara baada ya kuenguliwa katika nafasi hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Mouad Hajji kutoka marehemu Fahmy ambaye hadi anakumbwa na umauti alikuwa na umri wa miaka 36, alitangaza hadharani kuwa atachukua fomu za kuwania Urais wa CAF katika Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo utakaofanyika mwakani akitaka kupamba na Rais Ahmad Ahmad.

Kabla ya kuhudumu katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Caf, Fahmy alikuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 na kabla ya hapo alikuwa ni ofisa wa idara ya mashindano ya CAF kuanzia mwaka 2007 hadi 2015.

Fahmy hakuingia katika soka kwa bahati mbaya kwani amezaliwa katika familia iliyobobe katika uongozi wa mchezo huo kwani babu na baba yake wote wamewahi kuwa makatibu wakuu wa CAF.

Babu yake, Mourad Fahmy alikuwa Katibu Mkuu wa CAF kuanzia mwaka 1961 hadi 1982 na baba yake Moustafa Fahmy alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia 1982 hadi 2010.