Gor Mahia v AFC Leopards utamu wa Mashemeji Derby upo hapa

Muktasari:

Mechi ya leo ni ya kisasi kwa Leopards maarufu kama Ingwe, kwani rekodi zinaonyeshwa KOgalo wamekuwa wakiinyanyasa tangu mwaka 1968, Gor ilipokuwa na siku 40 tu tangu iasisiwe na ikashinda 2-1 dhidi ya Leopards iliyoanzishwa 1964.

UNAAMBIWA leo kabla ya Kariakoo Derby kupigwa pale Taifa, kule kwa majirani zetu Kenya kuna goma litapigwa mapema jioni wakati Gor Mahia na AFC Leopards zitakapokiwasha katika Mashemeji Derby.
Wapinzani hao wa jadi wa Kenya watavaana Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, jijini Nairobi ikiwa ni mechi ya marudiano baada ya ile ya kwanza iliyoisha kwa AFC kupigwa 4-1.
Mechi ya leo ni ya kisasi kwa Leopards maarufu kama Ingwe, kwani rekodi zinaonyeshwa KOgalo wamekuwa wakiinyanyasa tangu mwaka 1968, Gor ilipokuwa na siku 40 tu tangu iasisiwe na ikashinda 2-1 dhidi ya Leopards iliyoanzishwa 1964.
Kwa muda mrefu sasa, Leopards, imekuwa kibonde kwa Gor Mahia, kwani katika mechi tisa za mashemeji za hivi karibuni, Gor imeshinda mara saba na sare mbili, huku ikionyesha katika mechi tano za hivi karibuni, KOgalo imefungwa mabao matatu huku Ingwe ikifungwa 10.
Kipa wa Gor, Mtanzania David Kissu na mwenzake wa Ingwe, Mganda Benjamin Ochan, watakuwa na kibarua kigumu cha kuwazuia Elvis Rupia na Kenneth Muguna mtawalia.
Takwimu inaonesha kuwa, katika vikosi hivi viwili, Muguna na Rupia ni moto wa kuotea mbali, lakini pia Gor ina mashine nyingine Juma Balinya.
Kwenye orodha ya ufungaji bora, Muguna ambaye ni nahodha wa KOgalo, ndiye kinara wa mabao kwa klabu yake, akiwa na mabao nane huku Rupia akiwa na mabao tisa. Gor Mahia wanahitaji kuongeza gepu la pointi kati yao na Kakamega Homeboyz. Gor Inawazidi Homeboyz kwa pointi nne tu yaani mechi moja na sare moja.
Kocha wa Gor, Steven Polack anaingiza katika mechi ya leo akijua lazima apate ushindi ili aendelee kuwakimbia Homeboyz, maana zimebaki mechi 12 tu, lakini pia mpinzani wake Anthony Kimani anataka kushinda mechi yake ya kwanza kama Kocha wa Ingwe na kama hujui safari ya ubingwa inaanzia leo kwani Leopards wanaamini kama Gor watateleza wanaweza kubeba taji lao ya 14.
Makocha hao wametambiana, kila mmoja akiamini leo atashinda na kuiweka timu yake pazuri kwenye mbio hizo za ubingwa kwa msimu wa 2019-2020.