Extra Spesho: Meja Kunta kupostiwa na Swizz Beatz nako kwiyo

Sunday February 23 2020

Mwanaspoti, Extra Spesho, Meja Kunta, Swizz Beatz, Tanzania, muziki, Sengeli

 

By Amour Hassan

KIKI ya ‘kifo’ iliyofanywa na msanii wa singeli, Meja Kunta bado haijawaingia akilini watu wengi wakiwamo wasanii wakubwa nchini. Msanii huyo anayeinukia vyema (na timu yake) walitengeneza kiki mbaya ambayo ingeweza hata kuwapoteza wapendwa wao wenyewe, jambo ambalo lingewatafuna milele.  Mama yake mzazi Meja Kunta alizimia baada ya kusikia taarifa mwanaye amefariki dunia katika ajali ya gari akiwa safarini kwenda mkoani Tanga.
Wapo waliofananisha tukio hilo na ajali iliyochukua uhai wa nyota wa filamu na Bongo Fleva, Sharo Milionea aliyefariki dunia kwa ajali ya gari akiwa njiani kwenda kwao Tanga.
Katika mahojiano na kipindi cha FNL cha EATv juzi Ijumaa, rapa Ney wa Mitego alisisitiza mameneja wa Meja Kunta ni wa ovyo zaidi kupata kutokea nchini kwa kutengeneza kiki ya kifo cha msanii wao anayeinukia.
Rapa Ney anaamini Meja Kunta kapoteza sapoti kutoka kwa watu wengi sana kutokana na kitendo chake kile.Hata mkongwe wa Bongo Fleva, Madee, ambaye alikuwa wa kwanza kufika eneo la ajali Segera, Tanga, aliponda kitendo cha kambi ya msanii huyo kutengeneza kiki ya Meja Kunta alikufa, ilhali yeye alimwona na wakazumgumza japo alikuwa hajisikii vyema baada ya gari yao kuacha njia na kusererekea bondeni.Meneja wa msanii huyo akajitokeza kukanusha taarifa hizo alizotoa jana yake.
Aliomba radhi kwa wanafamilia, jamii, wanahabari na mashabiki wa msanii huyo kwa taarifa za uongo alizotoa kupitia ujumbe aliouposti kwenye ukurasa wake wa Instagram. Madee alimshauri Kunta kama msanii anayenukia, hapaswi kutafuta umaarufu kwa kiki.
‘Rais wa Manzese’ Madee alisema msanii anaweza kupoteza watu wanaomsapoti kwa kufanya vitu vya kuchefua kama kiki za aina hiyo.
“Kuna watu wanaweza kuwa walikupenda kwa kazi zako tu, lakini ukafanya jambo likawafanya wakuhame na kuamua kwenda kushabikia wasanii wengine,” alisema Madee alipohojiwa na Wasafi Tv baada ya ukweli wa tukio kubainika.
Waandaaji wa kipindi cha XXL cha Clouds FM walimpa Meja Kunta bonge la ‘interview’ la live kutokea studio kufafanua tukio hilo. Japo watangazaji walionyesha wazi kukerwa na kiki iliyofanywa na Kunta, ambayo ilizidi kudhihirika kutokana na timu yake kujiuma-uma katika kujibu maswali, lakini tayari Kunta alishakipata alichodhamiria na timu yake. Alitrendi kila kona kwenye mitandao ya kijamii na kupata ‘interviews’ ambazo isingekuwa rahisi kuzipata hapo kabla ya kiki yake. Kwenye safu hii ya ‘Extra Spesho’ ya Mwanaspoti Jumapili tulilichambua tukio lote chini ya kichwa cha habari ‘Ni kipaji sio kiki itakayokubeba Meja Kunta’.
Hakika ni kipaji tu ndiyo kinambeba msanii na wala sio kiki (kwani kuna mwenye kiki kumshinda Harmo Rapa?). Lakini kila mwanadamu anakosea. Kama Meja Kunta alikosea na keshaomba radhi kwa yaliyotokea ni wakati wa kumsamehe na kusonga mbele. Ni wakati wa Meja Kunta kuthibitisha ukubwa wa kipaji chake kama alivyofanya katika ngoma yake ya ‘Mamu’ ambayo remix yake alimshirikisha rapa Mr Blue, au hata alivyofanya katika ngoma yake ya ‘Haloo’.
Wiki hii anga la Bongo Fleva limetingishika baada ya mwanamuziki mkubwa wa Marekani, Swizz Beatz, ambaye pia ni prodyuza wa muziki na mume wa mwimbaji supastaa wa dunia, Alicia Keys, kuposti video ya ngoma inayotamba sasa ya Meja Kunta ya ‘Wanga (Wabaya)’ iliyomshirikisha nyota wa familia ya WCB, Lavalava. Sio kiki iliyomvutia Swizz Beatz kuposti video ya ngoma hiyo. Ni uzuri wa ngoma yenyewe. ‘Wanga (Wabaya)’ ni bonge ya ngoma, kama hujaisikia itafute uisikilize, utaniambia. Ni tamu kama kichombwezo cha wimbo huo kinachotrendi sasa cha “kuku kishingo kwiyo”.
Swizz Beatz ni gwiji wa muziki. Anajua ngoma kali inakuwa na vitu gani. Ngoma ya ‘Wanga’ ina kila kitu. Swizz aliposti pia ngoma kali mpya ya ‘Gere’ ya Diamond aliyoimba na baby mama wake, Tanasha Donna, huku Swizz akimWita “Simba kaka yangu.”
Ni kazi kama hizi Meja Kunta ambazo zitakudumisha kwenye gemu, siyo kiki.

Advertisement