Banda; Haikuwa rahisi Highlands Park kuing’oa Kaizer Chief

Muktasari:

Pamoja na kucheza kwa dakika zote za mchezo huo, Banda hakuwa miongoni mwa wachezaji wa Highlands Park ambao walihusika na katika upigaji wa mikwaju ya penalti.

KLABU ya Highlands Park anayoichezea beki wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda, imetinga robo fainali ya Kombe la Nedbank  Afrika Kusini baada ya kuing’oa  Kaizer Chiefs  kwa penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Makhulong.
Dakika 90 za mchezo huo, zilishindwa kuamua nani atakayevuka katika  hatua ya 16 bora baada ya kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Timu ya Banda ndio iliyokuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo huo kupitia kwa Peter Shalulile dakika ya  57,  Simba hao wa Kaskazini, walijikuta wakiwasawazishia wapinzani wao, baada ya dakika ya 63, Sello Motsepe.
Banda ambaye alicheza na Bevan Fransman kama mabeki pacha wa kati (4 & 5) walionekana kuwa na maelewano mazuri ambayo yaliwafanya kumzuia mshambuliaji hatari wa Kaizer Chiefs, Khama  Billiat licha ya  kushambulia akitokea pembeni.
Mzimbabwe huyo alishindwa kufurukuta mbele ya ukuta huo ambao Highlands Park katika dakika zote hadi zilipoongezwa 30 kabla ya kwenda katika mikwaju ya penalti ambayo iliamua mchezo huo.
Pamoja na kucheza kwa dakika zote za mchezo huo, Banda hakuwa miongoni mwa wachezaji wa Highlands Park ambao walihusika na katika upigaji wa mikwaju ya penalti.
Penalti za Highlands Park zilipigwa na Mzava, Mbatha aliyepoteza, Ramagalela, Shalulile, Fransman, Nyatama wote wakifunga kwa upande wa Kaizer, Cardoso, Mathoho, Manyama na Katsande ndio waliotupia huku Maluleka na Billiat wakipoteza.

MSIKIE  BANDA
Baada ya mchezo huo, Banda alisema walicheza kwa kuiheshimu Kaizer, hivyo walijitahidi kutofanya makosa ambayo yangeweza kuwagharimu kutokana na ubora wa wapinzani wao.
“Haikuwa kazi nyepesi kuiondoa Kaizer, tunajua ni miongoni mwa timu nzuri na bora Afrika, tulicheza kwa nidhamu,” alisema beki huyo.
Wakati huo huo, Bidvest Wits leo itakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Chippa United  katika mchezo wa mwisho wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Nedbank.