Andre Marriner : Mwamuzi aliyetibua mechi ya 1,000 ya Arsene Wenger

Tuesday March 24 2020

Mwamuzi aliyetibua mechi ya 1,000 ya Arsene Wenger,Andre Marriner,Arsene Wenger,kocha wa Arsenal,soka duniani ,

 

LONDON,ENGLAND. MACHI 22, mwaka 2014 ikiwa imepita takribani miaka sita sasa kuna mauaji yalitokea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge pale jijini London. Ndio, ilikuwa siku muhimu yenye kumbukumbu kwenye soka duniani wakati kocha wa Arsenal, Arsene Wenger na jeshi lake walikuwa uwanjani hapo kuikabili Chelsea.

Utamu zaidi wa mchezo huo ni kwamba, Wenger alikuwa anafikisha mchezo wake wa 1000 akiwa na kikosi cha washika bunduki hao wa London tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo. Halikuwa jambo dogo kabisa, mechi ya 1000.

Lakini, kilichotokea hata mwenyewe Wenger hakuamini kwani, alikutana kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 6-0. Hata hivyo, lawama nyingi zilimuendea mwamuzi wa kati, Andre Marriner na wasaidizi wake kwa kushindwa kusimamia vyema sheria hivyo, kutibua kila kitu kwa Wenger.

Katika mchezo huo, Marriner alimpa beki Kieran Gibbs kadi nyekundu badala ya Alex Oxlade-Chamberlain, ambaye ndiye alipaswa kuadhibiwa kwa kosa la kuunawa mpira makusudi. Ilikuwa ni kituko!

Uamuzi huo sio tu ulivuruga sherehe ya Wenger, bali uliuacha dunia na mshangao. Mwamuzi Clive Thomas katika kuonesha mshutuko wake, alilitaja tukio hilo kuwa ni la kukera na kushangaza.

Baadaye Wenger alisikika akisema huenda mwamuzi hakuona kilichotokea huku Kocha wa Chelsea (wakati huo), Jose Mourinho akilazimika kuomba msaada wa usaidizi wa mkanda wa video. Unajua kilichotokea baada ya madudu hayo. Wachezaji wa Arsenal walivurugwa!

Advertisement

Zilikuwa zimekatika dakika 15 tu, kabla ya tukio hilo wakati huo Arsenal walishapigwa bao 2-0, lakini walikuwa katika morali ya kupindua meza.

Baadaye ya hapo, wakaamua kujilinda maana walichanganyikiwa kwelikweli. Hata hivyo, katika kujilinda huko wakajikuta wanapigwa mabao manne ya haraka haraka.

Ilichukua dakika 20 tu kwa Chelsea kuwapiga Arsenal mabao manne na kufanya matokeo kuwa 6-0.

Supastaa wa Cameroon, Samuel Eto’o ndiye aliyepeleka kilio kwa kupachika bao dakika ya tano tu kabla ya Andre Schurrle kuongeza la pili. Eden Hazard na Fernando Torres wakapigiana pasi za kibabe na shuti hafifu likazuiwa kwa mkono na Oxlade-Chamberlain.

Lakini, kituko kikawa kwa Marriner ambaye aliamua kumpa kadi nyekundu Gibbs badala ya Chamberlain. Gibbs hakupinga kadi hiyo huyu taratibu akatoka nje ya uwanja. Hazard alifunga penalti hiyo huku Oscar akimalizia kazi aliyoianza kipindi cha kwanza kwa kufunga bao lake la pili, na la tano kwa Chelsea.

Msumari wa mwisho ukakwamishwa wavuni na Mohammed Salah, ambaye ndio kwanza alikuwa anachipukia. Huo ukawa mwisho wa maandalizi ya sherehe ya Wenger tena mbele ya mpinzani wake waliyewahi kushikana mashati, Mourinho. Imeandaliwa na Fadhil Athumani kwa msaada wa mitandao.

Advertisement