Mwalusako: Zahera hakuijua Yanga vizuri

Muktasari:

Zahera ametemwa Yanga ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo ilipoondoshwa katika mashindano ya kimataifa Jumapili iliyopita kwa kuruhusu kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Pyramids nchini Misri, awali ilifungwa 2-1 jijini Mwanza.

Dar es Salaam.Katibu mkuu wa zamani wa Yanga, Lawrance Mwalusako amesema kocha Mwinyi Zahera hakuifahamu vizuri Yanga.

Mwalusako aliyewahi kuichezea Yanga kabla ya kuwa kiongozi alisema alitambua kocha huyo hawezi kudumu Jangwani.

"Hakujua tabia ya watu wa Yanga, kuna wakati alikuwa akizungumzia hadi masuala ya uongozi na kuona kawaida.

"Hakuisoma Yanga ina watu wenye tabia gani, wanahitaji nini na aishi nao vipi.

Alisema hata kauli yake ya kwamba wachezaji waliosajili Yanga si wa mashindano ya kimataifa haikuwa sahihi kutamka vile.

"Yeye ndiyo alifanya usajili wa wale wachezaji kwa asilimia kubwa, kama hawakuwa wa mashindano ya kimataifa basi aliingiza 'mkenge' klabu katika usajili.

Alisema katika vitu ambavyo Yanga hawapendi ni kufungwa na ikitokea wamefungwa basi kuwe na sababu iliyojitosheleza hadi kufungwa na si kizembe," alisema Mwalusako.

Alisema kocha Zahera aliwaacha wachezaji kama Kamusoko ambao walikuwa vizuri bila sababu na kuwasajili wachezaji ambao baadhi yao hawajaonyesha kuisadia timu.